Miongoni mwa halmashauri zinazopiga
hatua kubwa katika sekta mbalimbali ni wilaya ya Kishapu ambayo inapatikana
mkoani Shinyanga, magharibi mwa Tanzania.
Kihistoria ilianzishwa rasmi Julai
2006 baada ya kuzaliwa na iliyokuwa Wilaya ya Shinyanga. Wilaya nyingine
zinazopatikana mkoani humo ni Msalala, Ushetu, Manispaa ya Shinyanga na Kahama.
Kishapu kwa nyakati tofauti imewahi
kuongozwa na wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi watendaji mbalimbali ambao
kwa nafasi zao wameweza kuleta kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali.
Sekta zinazopiga hatua wilayani humo pamoja na
kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni pamoja na elimu ambayo imegawanyika
katika makundi mawili kwa maana ya ile ya msingi na sekondari.
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo wilaya kwa nafasi
yake imekuwa ikitoa huduma za elimu kwa wananchi kupitia Idara ya Elimu ambayo
inaundwa na watumishi wenye taaluma hiyo ambao hufanya kazi kwa kuzingatia
weledi.
Hii ni idara ambayo ina umuhimu wake kwa kuwa ndiyo
jiko linalopika wataalamu mbalimbali wa baadaye ambao watakuwa ni tegemeo la
wazazi na taifa kwa ujumla kwani elimu ndio msingi wa maendeleo.
Katika makala haya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Wilson Nyamunda anazungumzia masuala
mbalimbali kuhusu sekta ya elimu ya msingi inavyopiga hatua pamoja na kugubikwa
na changamoto mbalimbali.
Kwa upande wa elimu ya msingi anabainisha kuwa wilaya
ina jumla ya shule 117 kati ya hizo 115 ni za Serikali na mbili ni za binafsi
ambapo moja inamilikiwa na Mgodi wa Williamson Diamonds na nyingine na Kanisa
la Anglikana.
Katika shule hizo jumla ya idadi ya wanafunzi
wanaosoma ni 44,556 na kati yao 23,384 ni wasichana na 21,172 ni wavulana huku ikielezwa
kuwa uandikishwa wa wanafunzi wa darasa la kwanza umepanda hadi asilimia 96.2
kufikia mwaka jana.
Kwa upande wa matokeo ya darasa la saba kaimu
mkurugenzi mtendaji huyo anabainisha mwaka jana jumla ya shule 116 kati ya 117
zilishiriki na kwamba ufaulu ulifikia asilimia 66.1 na kushika nafasi ya pili
kimkoa.
Waswahili wanasema usione vinaelea ujue vimeundwa na
ndivyo ilivyo kwa Kishapu, Nyamunda ambaye pia ni mwanasheria wa wilaya hiyo
anaweka wazi kuwa jitihada mbalimbali kama utaratibu wa utoaji uji pamoja na
wanafunzi kuwa na vipindi vya ziada ndiyo siri ya mafanikio.
“Lengo la asilimia ya ufaulu mwaka 2015 lilikuwa ni
60 lakini kwa kutumia jitihada za ufuatiliaji taaluma, walimu kulipwa stahiki
zao pamoja na darasa la saba kutokwenda likizo mwezi wa sita kumechangia wilaya
kuvuka hadi asilimia 66.1,” anasema.
Kutokana na mkakati wa Serikali kuhakikisha
wanafunzi wanakuwa na afya njema ili kufanya vizuzri darasani, wilaya
ikishirikiana na wafadhili pamoja na wadau mbalimbali wa elimu inatekeleza
mkakati huo.
Kwa mujibu wa Nyamunda hadi kufikia Desemba 2015 shule
za msingi 117 zilikuwa zinatoa uji kwa wanafunzi na kwamba miongoni mwake shule
tatu zitaendelea kupata ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Anataja shule hizo kuwa ni Mayanji iliyoko kata ya
Ukenyenge, Kakolo inayopatikana Uchunga pamoja na Bulimba ya kata ya Ukenyenge
ambazo zote zina uhakika wa kutoa chakula kwa wanafunzi hadi Juni 2016.
“Pamoja na hayo kuanzia Januari tunatarajia kuwepo
kwa changamoto ya ukosefu wa nafaka kwa shule zote kutokana na kutokuwepo kwa
mvua za kutosha msimu uliopita wa mwaka 2015, hii inafanya shule mbili zenye
uhakika wa kuendelea na zoezi la utoaji uji, shule hizo ni Mhunze kata ya
Kishapu na Busangwa iliyopo kata ya Busangwa,” anafafanua.
Changamoto zinazoikabili elimu ya msingi
Ni kawaida kizuri hakikosi kuwa na changamoto na
ndivyo ilivyo kwa wilaya ya Kishapu ambapo pamoja na mafanikio katika sekta ya
elimu bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa nyumba za walimu.
Nyamunda anabainisha kuwa kuna mahitaji ya nyumba
1059 lakini hadi sasa zipo 271 pekee ambazo ni sawa na asilimia 25.5 ya lengo
jambo ambalo huwafanya walimu wengi kukaa nje ya vituo hivyo kuchelewa kufika
kazini au kuchoka hali inayochangia ufubdishaji hafifu.
Mbali na upungufu wa nyumba za walimu pia vyumba vya
madarasa navyo havitoshelezi ambapo hadi sasa vipo 802 pungufu ya 1367 ya
mahitaji yote ambavyo ni sawa na asilimia 58.6 hali inayosababisha baadhi ya
wanafunzi kusoma nje ya madarasa.
“Upungufu wa vyumba vya madarasa katika elimu ya
msingi huchangia pia madarasa mawili kusomea chumba kimoja cha darasa kwa mfano
shule ya msingi Mwamagembe ina vyumba vinne pekee na pia upungufu wa madawati unatukabili,”
anasema,
Hata hivyo anasema kuwa baadhi ya walimu hawapendi
kufanya katika vituo vilivyo mbali na huduma za jamii na hivyo kuwafanya kuwa
na dharula na ruhusa nyingi hivyo kuna umuhimu wa kuwa na nyumba za watumishi
hao wa kada hiyo.
Wilaya inakabilianaje na changamoto?
Nyamunda anasema katika kukabiliana na changamoto
zza nyumba za walimu, wilaya imetenga kiasi cha sh. milioni 70 kwenye bajeti ya
mwaka 2015/2016 ambazo zitatumika kukamilisha ujenzi wa nyumba 16 za walimu.
Anataja shule hizo kuwa ni Lubaga, Seke, Mwaweja,
Lagana, Shagihilu, Bupigi, Ng’wanghili, Ikombabuki, Illa, Bubinza, Dugushilu,
Ng’wigumbi, Muguda, Ng’wajidalala, Ng’wamanota na Shiya.
Anaongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya
vyumba vya madarasa, wilaya imetenga sh. milioni 65 kwenye bajeti ya mwaka
2015/2016 zitakazotumika kukamilisha ujenzi wa vyumba 15.
“Kama wilaya tupo katika hatua za kuendeleza ujenzi
wa shule mpya za Mwatuju iliyoko kata ya Shagihilu na Mwangolomwa kata ya Seke
Bugolo, lakini pia tutawatumia wadau mbalimbali kama Benki ya Mgodi wa
Williamson, NMB, Taasisi ya Mwakasege na wengine kufadhili madawati pamoja na
TCRS watakaotusadia kujenga vyoo,” anadokeza.
Kwa mujibu wa Nyamunda, wilaya itasimamia matumizi
ya fedha vizuri ili zitumike kuleta tija kwa wanafunzi na walimu, kuhamasisha
kila shule kulima ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula mashuleni.
Pamoja na hayo, hivi karibuni wadau mbalimbali wa
elimu walikutana katika halmashauri ya wilaya hiyo na kuweza kubainisha
changamoto zinazochangia tatizo la ufaulu duni sambamba na kuboresha sekta
hiyo.
Kwa kuzingatia jitihada hizo wilaya inatarajia kuleta
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu ya msingi ambayo ndiyo daraja
la kuelekea sekondari na baadaye elimu ya juu hali inayochangia taifa lenye
ustawi.