Fundi akiwajibika katika kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi wilayani Kishapu. |
·
Serikali ya Awamu ya Tano iko katika mkakati wake kabambe
wa kuhakikisha kuwa Sera ya Tanzania yenye viwanda inafanikiwa, lengo kubwa likiwa
ni kukuza na kuinua uchumi wa nchi.
Yote hayo yanafanyika kwa kufufua viwanda mbalimbali ambavyo
vilikuwa vimekufa na kusitisha uzalishaji wake kutokana na sababu mbalimbali hatua
inayokwenda sanjari na kujenga vipya.
Tunashuhudia juhudi kubwa za Serikali zikizaa matunda
katika maeneo kadhaa ya taifa letu ambayo tayari wawekezaji wameanzisha viwanda
vya kutengeneza bidhaa mbalimbali.
Katika kudhihirisha hilo, pia Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inayoongozwa
na Waziri Charles Mwijage imejikita katika kuwezesha wajasiriamali ili wainuke
na kutambulika katika soko la kitaifa na kimataifa.
Hilo linafanyika kupitia maonesho mbalimbali ya viwanda
na biashara ambayo hufanyika kila mwaka lengo ni kuwapa fursa wajasiriamali hao
kuonesha bidhaa zao haijalishi kama ni kubwa au ndogondogo.
Katika hilo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iliyopo
katika Mkoa wa Shinyanga magharibi mwa Tanzania haiko nyuma kwani tayari
imeanza utekelezaji wa sera hiyo muhimu kwa ustawi wa nchi.
Wilaya hiyo kupitia kikundi cha Badimi inajivunia kuwa
na kiwanda kidogo cha kusindika na kutengeneza bidhaa za ngozi za wanyama
zikiwemo viatu, mikoba na mikanda.
Tayari wakazi wa Kishapu wameanza kuona matunda ya
kiwanda hicho kidogo ambacho kinatarajiwa kuwa nia mojawapo ya kujipatia
maendeleo siyo tu ya kikundi bali pia kwa taifa.
“Dhamira yetu ni
kutengeneza ajira kwa wanakikundi, kuwezesha fursa za kiuchumi miongoni mwa
wanakikundi na wananchi kwa ujumla waliomo ndani na nje ya Wilaya ya Kishapu,” ndivyo
anavyobainisha Said Luhende ambaye ni katibu wa kikundi hicho.
Akifafanua zaidi anasema neno Badimi likiwa linamaanisha
kundi la wafugaji ambao ni walinzi na wachungaji mifugo iliundwa Novemba 11,
2009 ikiwa na wanachama waanzilishi 10.
Kikundi hicho ambacho kina jumla ya wanachama 53 ambapo
27 kati yao ni wanaume na 26 ni wanawake, walianza kuuziana hisa, kusindika
ngozi na kuogesha mifugo shughuli walizoendelea nazo hadi kufikia hatua ya
kutengeneza bidhaa za ngozi.
Katibu huyo wa kikundi hicho anaendelea kudokeza kuwa malengo
hasa ya mradi au kiwanda hicho kidogo ni kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi ghafi
ndani na nje ya wilaya hiyo.
Idara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inaongozwa na Mkuu
wake, Dk. Alphonce Bagambabyaki akishirikiana na
wataalamu wake walioenea kata mbalimbali ndiyo wenye dhamana ya masuala yote ya
bidhaa za ngozi za mifugo mbalimbali.
Wilaya ya Kishapu ina idadi kubwa ya mifugo kwa ujumla
na ni kweli kuwa zao la ngozi litokanalo na mifugo halithaminiwi kwa kiwango
kinacholingana na thamani yake.
Kupitia idara hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kishapu inahakikisha inalifanya zao hilo la bidhaa za ngozi liwe linatambulika
na kuwa na thamani kubwa kwa mfugaji wa mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Kwa mujibu wa takwimu kwa wastani jumla ya ngozi za wanyama
kama ng’ombe 350, za mbuzi 800 na kondoo 280 huweza kupatikana kwa kila mwezi
ambazo zinaweza kusaidia utengenezaji wa bidhaa za kutosha.
Baadhi ya ngozi ambazo zimekuwa zikitupwa kutokana na
kukosa soko sasa zitakuwa zinaokolewa na wakati huo mfugaji kwa uapnde wake
atakuwa anapata faida kubwa kwa kujipatia kipato kutokana na mauzo ya ngozi
ghafi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Nyabaganga Taraba kwa upande wake anatoa
pongezi za dhati kwa kikundi hicho cha wajasiriamali cha Badimi na kusema kuwa
Kishapu ya viwanda inawezekana.
“Mara zote mwanzo huwa ni mgumu na mara nyingi huwa
tunapenda kushiriki pale ambapo tunaona matunda ya jitihada fulani yanatokea lakini
hatupendi kuonesha ushirikiano tangu mwanzo, hivyo sasa tufike mahali tutiane
moyo,” anasisitiza
Anawakaribisha Watanzania wanohitaji kujenga viwanda
wafike wilayani humo ili kuwekeza viwanda hatua itakayosaidia kuzidi kujenga
uchumi imara na kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa ajira.
Taraba anaendelea kusema kuwa yapo maeneo yaliyopimwa yakiwemo
Mwigumbi kwenye kata ya Bubiki ambayo yamekaa kibiashara na kimkakati hivyo
kuwa kichocheo kikubwa cha biashara.
Kwanini Mwigumbi?
Hili ni eneo ambalo kimsingi ni njia panda ya karibu
zaidi ya kwenda nchi jirani ya Kenya kwa barabara ambayo huweza kurahisisha
usafiri wa magari makubwa kama malori kusafirisha bidhaa.
Si hivyo tu bali pia ni njia panda ya kwenda mikoa
jirani kama Simiyu, Mara, Manyara na Arusha hivyo kuwa kitovu kizuri cha
biashara hali inayoweza kufanya mzunguko mkubwa wa fedha wilayani Kishapu.
Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli alizindua mradi wa
ujenzi wa barabara kuu ambayo itaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Simiyu hatua
itakayorahisha na kupunguza usafirishaji kwenda Kenya.
Itakumbukwa pia Mwigumbi ni eneo ambalo linatarajiwa
kupitiwa na reli ya kasi ya ‘standard garge’ hivyo mkuu huyo wa wilaya
anawakaribisha wawekezaji kujenga bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya
maeneo ya jirani.
Maeneo mengine ya uwekezaji
Mbali ya Mwigumbi, Taraba anabainisha wilaya hiyo
imejaliwa maeneo mengine ya uwekezaji kama mji mdogo wa Kishapu na mengine
yakiwemo Nyasamba kwenye kata ya Bubiki, Mipa kata ya Mondo, Uchunga,
Ukenyenge, Bunambiyu pamoja na Igaga.
Pamba ndilo zao kuu la biashara linalotambulika katika
wilaya hiyo lakini ukweli ni kuwa yapo mazao mengine yanayofanya vizuri na
kuwainua wakulima yakiwemo mkonge, alizeti na dengu.
Anaagiza kila kata kubainisha fusra zisizopungua tatu
ambazo wanaona kutokana na mazingira yanayowazunguka na kutoa rasilimali watu
zinaweza kuchangia uanzishwaji wa viwanda.
Anasema lengo ni kuzitambua fursa hizo na hivyo kuanza
michakato mapema ya kujenga viwanda wenyewe bila kutegemea wawekezaji kutoka
nje kufika Kishapu na kuvijenga.
Mkuu wa wilaya anawakaribisha wawekezaji kuwekeza
katika mazao hayo kwa kujenga viwanda kwa ajili ya kukamua alizeti kupata
mafuta ya kupikia, kusindika mkonge na kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na
sabuni.
Anasema pamoja na hayo ni dhahiri kuwa viwanda
havitajengwa na watu wa nje bali vitajengwa na wananchi wazawa kwa kutumia
malighafi zinazopatikana ndani katika maeneo wanayoishi.
Kwa kutumia wananchi waliomo ndani wenye ujuzi tofauti
tofauti au waliosomea katika vyuo mbalimbali na kupata mafunzo au wenye kuwa na
ubunifu ambao unaweza kuleta mapinduzi ya viwanda.
Hivyo Kishapu ya viwanda inawezekana jambo muhimu ni
wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuendelea kujenga uchumi
imara kama ilivyo kaulimbiu ya halmashauri ya wilaya hiyo.