Sunday, April 9, 2017

MKUU WA WILAYA ATOA TAHADHARI YA NDEGE KWELEA

Mkuu wa wilaya Kishapu akizungumza na wananchi

MKUU WA WILAYA ATOA TAHADHARI YA NDEGE KWELEA

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewataka wananchi wilayani humo kuchukua tahadhari na baa la ndege waharibifu wa mazao mashambani aina ya kwelea.

Amesema tayari baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo yamevamiwa na ndege hao waharibifu wa mazao yakiwemo ya mtama, uwele, alizeti na mahindi yanayoanza kustawi.

Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alitoa tahadhari hiyo kwa wananchi mwishoni mwa wiki alipofanya ziara ya katika vijiji vya kata sita zilizopo wilayani humo.

Akiwa amembatana na Ofisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji Wilaya, George Kessy na Ofisa Nyuki na Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya (OCD), Emmanuel Gariyamoshi aliwatembelea wananchi wa kata za Uchunga, Mwadui Lohumbo, Idukilo, Ukenyenge, Mwamasele na Mwaweja.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kulinda mashamba yao na kuwafukuza ndege hao wakati Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka ili kuwasaidia.

Alisema tayari wilaya imeagiza ndege maalumu kwa ajili ya kumwaga sumu kwenye mazalia ya ndege hao ili wasiongezeke na kuleta madhara zaidi kwa mashamba ya wananchi.

“Serikali haijawatupa nawaomba wananchi tukae mashambani mwetu tulinde na kuwafukuza ndege hao wasile mazao yetu kwani tutapata hasara kubwa, hatujui hao kwelea kwelea watakuja lini, na hatujui hiyo ndege itakuja lini,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi kuvuna haraka iwezekanavyo mazao ambayo tayari yamekomaa ili kutowapa mwanya ndege hao kufanya uharibifu wao na hivyo kuwapa hasara wakulima.

Aliwataka wakulima wasihadaiwe na kuuza mazao yote kwa wafanyabiashara hali inayoweza kuwasababishia kukosa chakula baadaye na kulazimika kununua chakula kwa bei ya juu.

Aliwaonya watu wanaofanya hivyo kwani huwaacha nyuma wakulima waliotoka jasho kulima mazao wakati wao wakineemeka kwa kuyauza mazao hayo kwa bei ya juu na kupata faida.

Kwa upande wake, Kessy alisema idara yake inawasisitizia wananchi wajenge utamaduni wa kuhifadhi chakula cha kutosha ghalani ili kiwasaidia katika siku zijazo na kuuza tu ile ziada inayobaki baada ya kutosheka.

Aliwapa mbinu za kufukuza kwelea kwelea kwa kuweka vitambaa mithili ya bendera, sanamu za watu na kupiga madebe ili kuwafukuza ndege hao ili wapiti mbali ya mashamba wasiweze kufanya uharibu.

Kwelea ni ndege ambao hupatikana Afrika pekee na hula mbegu za nyasi pori na pia nafaka, kama vile mtama, mchele na ngano pamoja na wadudu wadudu waharibifu wa mazao.

Mbinu za udhibiti ni pamoja na unyunyizaji wa dawa yenye sumu lakini pia ushirikiano wa wakulima zikiwemo kuwatisha ndege kwa silaha za kujitengeneza zitumiazo mawe.