Wednesday, May 10, 2017

DC Kishapu azindua Baraza la Biashara


Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewataka Watanzania kupenda kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kwenda sambamba na sera ya Tanzania yenye viwanda pamoja na kuimarisha uchumi wetu.
Amesema hayo wakati akizindua Baraza la Biashara Wilaya ambapo alishangazwa na baadhi ya watu kuamini kuwa bidhaa zinazozalishwa nchini hazina ubora na hivyo kukimbilia za nje.
Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Biashara Wilaya alisema bidhaa zetu zina ubora kutokana na kutumia malighafi halisi akitolea mfano viatu vinavyozalishwa na Watanzania ukilinganisha na vinavyotoka nje ya nchi ambavyo vingi havidumu.
”Tufike mahali sasa tununue bidhaa zetu ili fedha izunguke kwani tutaimarisha uchumi na kama tunavyofahamu lengo la Rais katika sera ya nchi ya viwanda anataka tununue bidhaa zetu.
Mkuu huyo wa wilaya alilitaka baraza liwe chachu ya kusukuma sera ya nchi ya viwanda na kuibua fursa ambazo wananchi waananchi wanaweza kuzitumia na kuanzisha biashara.
Alilitaka baraza kuja na wazo mbadala la kibishara na kiviwanda ili wananchi waweze wawaunga mkono wajasirimali wadogo wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa wapate masoko.
Akifungua kikao cha kwanza cha baraza hilo, Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Barazaa la Biashara Wilaya, Stephen Magoiga aliwataka wananchi kutumia vizuri fursa zilizopo wilayani humo.
Magoiga ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu alisema tukitumia vizuri rasilimali zilizopo wilayani humo tutapiga hatua na kujenga historia.
”Tunapozungumzia viwanda siyo lazima viwe vikubwa hata vidogo vidogo mfano tunaweza kutumia kilimo kuibadilisha kabisa Kishapu na kuwa wilaya ya kwanza katika uchumi,” alisema.
Alitaja rasilimali kama madini na fursa za kilimo zilizopo wilayani humo kuwa kama zikitumika ipasavyo maisha ya wananchi yataboreka zaidi na uchumi kwa ujumla kuimarika.
Baraza hilo la biashara Wilaya ya Kishapu linaundwa na wajumbe 40 wakiwemo wawakilishi kutoka sekta ya umma na binafsi na litadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.