Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameagiza wananchi
kuendelea kuelimishwa kuhusu athari zinazotokana na vitendo vya ukataji miti
ovyo.
Alitoa agizo hilo juzi katika hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba wakati wa kilele cha
Wiki ya Mazingira Duniani iliyoadhmishwa kimkoa kijiji cha Mwamashele wilayani
hapa.
Alisema wananchi wengi wanakosa uelewa kuwa vitendo vya
ukataji miti vinatishia uhai wa binadamu na wanyama hali inayotokana na ukosefu
wa mvua na hivyo kusababisha ukame.
Telack alifafanua kuwa misitu ndiyo mhimili mkubwa wa
kulinda mazingira yetu na kutupatia nishati, dawa za asili, vifaa vya ujenzi
pamoja na kuboresha hali ya hewa.
“Pamoja na umuhimu wake kwa binadamu na mazingira misitu
imekumbwa na uharibifu mkubwa katika mkoa wetu wa Shinyanga kwa matumizi
mbalimbali yakiwemo ya uchomaji mkaa,” alisema.
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa uchomaji wa mkaa
katika maeneo mengi kama vile Nyasamba wilayani hapa umekuwa kama shughuli ya
kujipatia kipato na hivyo kutishia kutoweka kwa misitu.
Hivyo aliwataka wadau kutumia nishati mbadala kama vile
vinyeshi vya wanyama pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi hayo
kwani matumizi ya mkaa ni adui wa mazingira.
Telack alionya kuwa uchomaji mkaa na utumiaji wake huongeza hewa ya ukaa
na kusababisha mabadiliko ya tabia ya nchi na hatimaye kuleta ukame.