Serikali
inatekeleza dhamira yake ya kuhakikisha inawapa wananchi huduma bora kwa wakati
na ufanisi ili kuboresha maisha yao kielimu, kiafya na kiuchumi.
Hayo
yanafanyika kwa ushurikiano mkubwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka
ndani na nje ya nchi ili kufanikisha utoaji huo wa huduma hizo muhimu za
kijamii.
Inatoa
kipaumbele katika huduma za afya na elimu zenye ubora na zinazowafikia wananchi
wote ili kuboresha maisha yao kwani afya na elimu bora kwa wananchi ndiyo
raslimali muhimu kwa maendeleo.
Maendeleo
ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na elimu na wenye
uwezo wa kuzalisha mali. Katika kuhakikisha hilo Serikali imeendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma
za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Hivi
karibuni Serikali ilizindua mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma au Public
Sector Systems Strengthening (PS3) ukiwa na lengo kusaidia kufanikisha utoaji
huduma bora hasa kwa wananchi walioko maeneo ya pembezoni.
Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia ufadhili wa
Shirika la Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID) inatekeleza mradi huo
ikishirikiana na wizara zinazosimamia sekta za afya, elimu na rasilimali fedha.
Utekelezaji
wa mfumo huo unaolenga kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya na elimu, unatarajiwa kuanza rasmi Julai 2017 katika vituo vyote
vya kutolea huduma za afya na elimu ambavyo vipo mikoa 13 inayotekeleza mradi
huo.
Katika
utoaji huduma hizi mashuleni au vituo vya kutolea huduma za afya vikiwemo
hospitali au zahanati suala la matumizi ya rasilimali fedha halikwepeki.
Hii
ni kutokana na umuhimu wake kwani ni sehemu ambazo hufanyika manunuzi
mbalimbali yakiwemo ya vitendea kazi vya kufundishia, kujifunzia, vya kutolea
tiba na dawa.
Hivyo
ni muhimu kuwepo na usimamizi wa mzuri ili kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa
na Serikali kuwahudumia wananchi zinatumika kwa usahihi kwa maana ya ‘value for
money’.
Kupitia mfumo huo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa au Facility Financial
Accounting and Reporting System (FFARS) utasaidia utekelezaji wa utoaji wa
rasilimali fedha moja kwa moja vituo vya kutolea huduma.
Hii ni katika
kuimarisha uhitaji wa kuwepo kwa usimamizi wa fedha katika ngazi ya vituo vya
kutolea huduma hizo za afya na elimu katika maeneo mbalimbali ya halmashauri.
Mfumo wa FFARS utaweza kuwapatia watoa huduma mfumo rahisi
ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika
vituo vyao.
Hivyo ufuatiliaji matumizi ya fedha hizo utakuwa
rahisi katika kufikia malengo ya utoaji huduma na kuhakikisha yanaendana na
sheria za ununuzi na utoaji taarifa.
Taarifa hizi zitasaidia Serikali kuimarisha mfumo wa
usimamizi wa fedha za umma na kuongeza uwazi hivyo watoa huduma watawajibika
kwa na wajibu kwa jamii wanayoihudumia.
Mfumo utatumika katika vituo vyote vya kutolea
huduma ya afya na shule, na uhuishaji huu wa mfumo utarahisishia na kuongeza
ufanisi katika mifumo ya Serikali ya Tanzania na kuboresha usimamizi na
matumizi ya rasilimali za umma.
Ili
kuhakikisha watoa huduma hizo muhimu, wadau ambao ni watoa huduma za afya na
elimu hivi karibuni walipatiwa mafunzo mahsusi ili kuwajengea uwezo katika
uhasibu na utoaji taarifa (FFARS).
Kwa kuanzia, Serikali
inatarajia kuanza kuutekeleza mfumo mfumo huo mikoa 13 katika halmashauri zake
93 ambapo Shinyanga ni miongoni mwa mikoa hiyo kupitia halmashauri zake zote
sita.
Katika
makala haya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen
Magoiga iliyonufaika na mradi huo anazungumzia kwa kina kuhusu mfumo wa FFARS.
Anatanabaisha
kuwa unasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi katika hesabu za mapato na
matumizi katika halmashauri zetu tofauti na ilivyokuwa zamani.
Magoiga
anasema kuwa kuundwa kwa mfumo huu kutasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku
zinasimamiwa vizuri na taarifa za matumizi yake zinatolewa kwa usahihi.
Anaongeza
kuwa utaratibu huu mpya utakuwa ni kichocheo cha uwazi na uwajibika wa
watendaji wa Serikali ambao ndio watoji wa huduma katika sekta za afya na elimu
kwa wananchi.
Hii
ni kutokana na kuwa vituo hivyo vya kutolea huduma vinakuwa na mfumo maalumu wa
kuandaa taarifa za mapato na matumizi tofauti na ilivyokuwa zamani.
Ni
dhahiri kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kutoa hudumia bora kwa wananchi wake
kwa ufanisi na hilo ndilo lengo lake linalotarajiwa kupitia fedha hizo.
Mkurugenzi
mtendaji huyo anasema ni kweli kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa
sahihi za rasilimali fedha katika vituo vya huduma.
Anasema
kuwa kutokana na changamoto hiyo halmashauri hushindwa kutoa taarifa sahihi za
matumizi ya ruzuku zinazotolewa katika vituo hivyo na wakati mwingine
kusababisha hamashauri husika kupata hati ya mashaka kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
“Awali
hakukuwa na mfumo sahihi wa kusaidia kulizuia hilo lakini kwa mfumo huu mpya
sasa utasaidia kuhakikisha kunakuwa na muundo maalumu wa kuhifadhi taarifa za
mapato na matumizi.
“Naamini
hii itaongeza uwazi na uwajibikaji wa vituo hivi vya kutolea huduma na hivyo
kupunguza changamoto mbalimbali ambazo zilikuwepo awali,” anasema.
Mfumo
huo kielektroniki ili kuendana na wakati na mabadiliko ya teknolojia ambapo
unafanya kazi sambamba ujazaji vitabu ulioboreshwa.
Hii
ni katika kuweza kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo umeme na
kutokuwa na upatikanaji wa mtandao kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma
katika halmashauri mbalimbali.
Aidha,
mara baada ya kujaza katika vitabu, takwimu hizo zitaingizwa katika mfumo
kwenye ngazi ya Halmashauri na vituo kupatiwa taarifa ya vituo vyao.
Ni
dhahiri kuwa vituo hivyo vitatoa taarifa sahihi ya mapato na matumizi ambazo
zitasaidia mwananchi kuhoji pale atakapoona kuwa huduma zinazotarajiwa
kupatikana katika vituo hazitolewi kulingana na ruzuku iliyotolewa.
Mradi
wa PS3 umefanikishwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto.