Friday, March 9, 2018
RC Ndikilo;Halmashauri Tengeni Fedha kuwawezesha Wanawake
Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mhandisi Evarist Ndikilo ametoa agizo kwa Halmashauri zote za mkoa wa Pwani kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kutoa asilimia tano ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi,maagizo hayo ameyatoa leo katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Mji wa Chalinze.
Mheshimiwa Ndikilo katika hotuba yake aliendelea kusisitiza kwamba wakati tukielekea kwenye Tanzania ya viwanda hatuna budi kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kupambana na umasikini na kuzalisha kwa tija kwani katika familia wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa na walezi wa familia.
Sanjari na kuwawezesha wanawake kiuchumi Mkuu wa Mkoa amekemea ndoa za utotoni,ukatili wa kijinsia kwa wanawake na kupambana na tamaduni zisizofaa zinazoweza kupelekea kukwamisha ndoto za mwanamke katika jamii na kushindwa kufikia malengo yake.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze,Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kwamba kwa Halmashauri ya Chalinze tunatekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi na maagizo ya serikali kwa Ujumla kwa kutenga fedha kwa ajili ya wanawake kwani kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 tulitenga fedha na kuwakopesha wanawake na Vijana kiasi cha milioni 234 na walikopeshwa zaidi ya asilimia 100 na wanawake wanajitahidi kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na aliwapongeza wakina mama kwa uaminifu huo na kuwataka jamii iendelee kuwatia moyo akina mama,Aidha kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmsahauri ya Chalinze imekwisha kopesha wanawake zaidi ya Milioni 120.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Mheshimiwa Said Zikatimu alipokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na kumhakikishia kuwa Halmashauri yake iko mstari wa mbele katika utengaji wa fedha kwa ajili ya Vijana na kuahidi kutoa fedha zingine kwa ajili ya mikopo ya wanawake na Vijana kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambazo zitakuwa Milioni 140
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii,Saidi Mwakapugi alitoa ufafanuzi kwa kueleza idadi ya vikundi vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ni 384 ,vikundi 215 ni vya wanawake na 169 ni vya vijana.Vikundi 59 vya wanawake na vikundi 50 vya vijana vilikopeshwa Jumla ya fedha za kitanzania Milioni 234 kwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na Jumla ya fedha za kitanzania Milioni 120 zimekopeshwa kwa wanawake na Vijana kwa mwaka huu wa 2017/2018.”Kwa mwaka 2016/2017 Halmashauri ilitoa fedha zote zilizokuwa zimetengwa kwa mujibu wa bajeti na kuzikopesha kwa walengwa au wanawake na vijana”Mwakapugi alisema.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo aliendelea kufafanua kwamba kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Chalinze imetenga Jumla ya fedha za kitanzania milioni 270 kwa ajili ya wanawake na vijana.