Tuesday, March 21, 2017

KISHAPU INAVYOBORESHA SEKTA YA ELIMU



Miongoni mwa halmashauri zinazopiga hatua kubwa katika sekta mbalimbali ni wilaya ya Kishapu ambayo inapatikana mkoani Shinyanga, magharibi mwa Tanzania.
Kihistoria ilianzishwa rasmi Julai 2006 baada ya kuzaliwa na iliyokuwa Wilaya ya Shinyanga. Wilaya nyingine zinazopatikana mkoani humo ni Msalala, Ushetu, Manispaa ya Shinyanga na Kahama.
Kishapu kwa nyakati tofauti imewahi kuongozwa na wakuu wa wilaya pamoja na wakurugenzi watendaji mbalimbali ambao kwa nafasi zao wameweza kuleta kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali.
Sekta zinazopiga hatua wilayani humo pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni pamoja na elimu ambayo imegawanyika katika makundi mawili kwa maana ya ile ya msingi na sekondari.
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo wilaya kwa nafasi yake imekuwa ikitoa huduma za elimu kwa wananchi kupitia Idara ya Elimu ambayo inaundwa na watumishi wenye taaluma hiyo ambao hufanya kazi kwa kuzingatia weledi.
Hii ni idara ambayo ina umuhimu wake kwa kuwa ndiyo jiko linalopika wataalamu mbalimbali wa baadaye ambao watakuwa ni tegemeo la wazazi na taifa kwa ujumla kwani elimu ndio msingi wa maendeleo.
Katika makala haya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Wilson Nyamunda anazungumzia masuala mbalimbali kuhusu sekta ya elimu ya msingi inavyopiga hatua pamoja na kugubikwa na changamoto mbalimbali.
Kwa upande wa elimu ya msingi anabainisha kuwa wilaya ina jumla ya shule 117 kati ya hizo 115 ni za Serikali na mbili ni za binafsi ambapo moja inamilikiwa na Mgodi wa Williamson Diamonds na nyingine na Kanisa la Anglikana.
Katika shule hizo jumla ya idadi ya wanafunzi wanaosoma ni 44,556 na kati yao 23,384 ni wasichana na 21,172 ni wavulana huku ikielezwa kuwa uandikishwa wa wanafunzi wa darasa la kwanza umepanda hadi asilimia 96.2 kufikia mwaka jana.
Kwa upande wa matokeo ya darasa la saba kaimu mkurugenzi mtendaji huyo anabainisha mwaka jana jumla ya shule 116 kati ya 117 zilishiriki na kwamba ufaulu ulifikia asilimia 66.1 na kushika nafasi ya pili kimkoa.
Waswahili wanasema usione vinaelea ujue vimeundwa na ndivyo ilivyo kwa Kishapu, Nyamunda ambaye pia ni mwanasheria wa wilaya hiyo anaweka wazi kuwa jitihada mbalimbali kama utaratibu wa utoaji uji pamoja na wanafunzi kuwa na vipindi vya ziada ndiyo siri ya mafanikio.
“Lengo la asilimia ya ufaulu mwaka 2015 lilikuwa ni 60 lakini kwa kutumia jitihada za ufuatiliaji taaluma, walimu kulipwa stahiki zao pamoja na darasa la saba kutokwenda likizo mwezi wa sita kumechangia wilaya kuvuka hadi asilimia 66.1,” anasema.  
Kutokana na mkakati wa Serikali kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na afya njema ili kufanya vizuzri darasani, wilaya ikishirikiana na wafadhili pamoja na wadau mbalimbali wa elimu inatekeleza mkakati huo.
Kwa mujibu wa Nyamunda hadi kufikia Desemba 2015 shule za msingi 117 zilikuwa zinatoa uji kwa wanafunzi na kwamba miongoni mwake shule tatu zitaendelea kupata ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani (WFP).
Anataja shule hizo kuwa ni Mayanji iliyoko kata ya Ukenyenge, Kakolo inayopatikana Uchunga pamoja na Bulimba ya kata ya Ukenyenge ambazo zote zina uhakika wa kutoa chakula kwa wanafunzi hadi Juni 2016.
“Pamoja na hayo kuanzia Januari tunatarajia kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa nafaka kwa shule zote kutokana na kutokuwepo kwa mvua za kutosha msimu uliopita wa mwaka 2015, hii inafanya shule mbili zenye uhakika wa kuendelea na zoezi la utoaji uji, shule hizo ni Mhunze kata ya Kishapu na Busangwa iliyopo kata ya Busangwa,” anafafanua.

Changamoto zinazoikabili elimu ya msingi
Ni kawaida kizuri hakikosi kuwa na changamoto na ndivyo ilivyo kwa wilaya ya Kishapu ambapo pamoja na mafanikio katika sekta ya elimu bado kuna changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa nyumba za walimu.
Nyamunda anabainisha kuwa kuna mahitaji ya nyumba 1059 lakini hadi sasa zipo 271 pekee ambazo ni sawa na asilimia 25.5 ya lengo jambo ambalo huwafanya walimu wengi kukaa nje ya vituo hivyo kuchelewa kufika kazini au kuchoka hali inayochangia ufubdishaji hafifu.
Mbali na upungufu wa nyumba za walimu pia vyumba vya madarasa navyo havitoshelezi ambapo hadi sasa vipo 802 pungufu ya 1367 ya mahitaji yote ambavyo ni sawa na asilimia 58.6 hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kusoma nje ya madarasa.
“Upungufu wa vyumba vya madarasa katika elimu ya msingi huchangia pia madarasa mawili kusomea chumba kimoja cha darasa kwa mfano shule ya msingi Mwamagembe ina vyumba vinne pekee na pia upungufu wa madawati unatukabili,” anasema,
Hata hivyo anasema kuwa baadhi ya walimu hawapendi kufanya katika vituo vilivyo mbali na huduma za jamii na hivyo kuwafanya kuwa na dharula na ruhusa nyingi hivyo kuna umuhimu wa kuwa na nyumba za watumishi hao wa kada hiyo.


Wilaya inakabilianaje na changamoto?
Nyamunda anasema katika kukabiliana na changamoto zza nyumba za walimu, wilaya imetenga kiasi cha sh. milioni 70 kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016 ambazo zitatumika kukamilisha ujenzi wa nyumba 16 za walimu.
Anataja shule hizo kuwa ni Lubaga, Seke, Mwaweja, Lagana, Shagihilu, Bupigi, Ng’wanghili, Ikombabuki, Illa, Bubinza, Dugushilu, Ng’wigumbi, Muguda, Ng’wajidalala, Ng’wamanota na Shiya.
Anaongeza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya vyumba vya madarasa, wilaya imetenga sh. milioni 65 kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016 zitakazotumika kukamilisha ujenzi wa vyumba 15.
“Kama wilaya tupo katika hatua za kuendeleza ujenzi wa shule mpya za Mwatuju iliyoko kata ya Shagihilu na Mwangolomwa kata ya Seke Bugolo, lakini pia tutawatumia wadau mbalimbali kama Benki ya Mgodi wa Williamson, NMB, Taasisi ya Mwakasege na wengine kufadhili madawati pamoja na TCRS watakaotusadia kujenga vyoo,” anadokeza.
Kwa mujibu wa Nyamunda, wilaya itasimamia matumizi ya fedha vizuri ili zitumike kuleta tija kwa wanafunzi na walimu, kuhamasisha kila shule kulima ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula mashuleni.
Pamoja na hayo, hivi karibuni wadau mbalimbali wa elimu walikutana katika halmashauri ya wilaya hiyo na kuweza kubainisha changamoto zinazochangia tatizo la ufaulu duni sambamba na kuboresha sekta hiyo.
Kwa kuzingatia jitihada hizo wilaya inatarajia kuleta Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu ya msingi ambayo ndiyo daraja la kuelekea sekondari na baadaye elimu ya juu hali inayochangia taifa lenye ustawi.