Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani amezindua
mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu katika mkoa wa Shinyanga
wilayani Kishapu wenye thamani ya sh. bilioni 35.5.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kijiji cha Negezi kata ya
Ukenyenge wilayani Kishapu,ukihusiha vijiji 149, Dk. Kalemani aliagiza Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikishwa wanasambaza umeme sehemu zote bila
upendeleo.
Aliwahimiza wananchi kutumia fursa ya kuwepo kwa nishati hiyoi
katika kuboresha maisha yao kwa kutumia miradi ya uzalishaji mali pamoja na
huduma mbalimbali za kijamii.
Aliwataka wautumie kwa kujenga viwanda vya kusindika mazao
pamoja na huduma za afya, elimu, maji na viwanda vingine kama mashine za kusaga
ambazo zitawapatia kipato na kuboresha maisha.
Aidha, naibu waziri huyo alizitaka serikali za kata na vijiji
kubainisha maenbeo maalumu ya viwanda ambayo katika mradi huo yatafikishiwa
miundombinu ya umeme mkubwa.
”Tunataka kuwezesha wajasriamali vijijini kupatiwa umeme
utakaowezseha kuanzishwa kwa viwanda vidogo na vikubwa vijijini kwa gharama
nafuu,” alisema Dk. Kalemani.
Aliongeza kuwa wananchi watakaounganishiwa umeme wanatakiwa
kukamilisha utandazaji wa nyaya katikia nyumba zao mapema ili mkandarasi
akifika wawe tayari kulipia na kuunganishiwa umeme.
Alisema kwa sehemu ambazo utandazaji utakuwa haujakamilika au
nyumba si kubwa wanahimizwa kuomba kufungiwa kifaa cha Umeme Tayari (UMETA)
ambacho hakihitaji kutandaza nyaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba
aliishukuru Serikali kwa mradi huo wa REA huku akisema utasaidia kutengeneza
ajira wilayani humo.
Taraba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Zainab Telack alisema nishati ya umeme vijijini itasaidia kuanzishwa kwa
viwanda vidogo na vya kati hivyo aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo na
kuacha uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo, alitoa kilio chake kwa kumuomba naibu waziri
kushughulikia changamoto ya baadhi ya wakandarasi kutomaliza miradi kwa wakati
jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo.
Pia mkuu huyo wa wilaya aliwaomba wananchi watoe ushirikiano kwa
kutoa maeneo kwa ajili ya kupitisha miundombinu ya umeme kwa kuwa ni kujiletea
maendeleo yao wenyewe.
Aliomba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa
Shinyanga kutatua kero ya kukatika kwa umeme mara kwa jambo ambalo limekuwa ni
kero kwa wananchi na linarudisha nyuma maendeleo.
Utekelezaji wa mradi huo ulianza Februari 2017 na
unatarajiwa kukamilika Machi 2019 ambapo tayari sh. bilioni 7.4 zimetumika
katika awamu ya kwanza wakati awamu ya pili jumla ya sh. bilioni 22.95
zilitumika.