MKURUGENZI wa Idara ya Habari MAELEZO, ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania, (BoT) kwa kuandaa mafunzo kwa waandishi wa habari za Uchumi na Fedha, yaliyomalizika mjini Unguja, Zanzibar jana Machi 31, 2017.
Dkt. Abaasi alisema, BoT, kama taasisi ya serikali inao wajibu wa kuwapatia habari wananchi kupitia waandishi wa habari na uamuzi wa kutoa mafunzo hayo ni ishara tosha ya ushirikishaji wa waandishi katika kuhakikisha wananchi wanapatiwa habari sahihi kutoka BoT na taasisi zingine za kiuchumi na fedha.
"Tumekutana hapa wakati serikali imepitisha sheria mbili, moja ni ile inayohusu huduma za vyombo vya habari, na ya pili ni ile ya haki ya waandishi kupata taarifa kutoka taasisi za serikali na mimi nikiwa kama msimamizi mkuu katika eneo hili la utoaji habari kwenye taasisi za umma, ninawaalika mtusumbue sana katika kupata taarifa maana utoaji wa habari kwa sasa si suala la utashi tena bali ni la kisheria." Alisema Dkt. Abbassi.
Dkt. Abbasi pia aligusia wajibu wa waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao chini ya sheria ya sasa,
“Lengo la sheria hii ni kuwajengea heshima Waandishi wa habari ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira ya heshima na bora, tofauti na hivi sasa ambapo taaluma ya uandishi wa habari imekuwa ikilalamikiwa kwa kuchafuliwa na baadhi ya waandishi ambao kimsingi hawana sifa za kuwa waandishi wa habari.” alisema na kuongeza,
“kila taaluma, iwe taaluma ya Sheria, iwe taaluma ya udaktari, lazima wote walio kwenye taaluma hizo wanasimamiwa na kanuni na sheria, kwa hivyo sheria hii itatenganisha kati ya waandishi wana taaluma na wale ambao si wana taaluma.” Alisema.
Dkt. Abbasi pia amekanusha habari kuwa Serikali kupitia sheria hii inataka kuwazuia baadhi ya watu wasifanye kazi za uandishi kwa kigezo cha kitaaluma.
“Hii si kweli, hata Yule anayeitwa Kanjanja, anaweza kufanya kazi ya uandishi lakini kwa kuzingatia kanuni mpya zinazoangazia sheria hii mpya, hivyo hata wale ambao si wanataaluma na wanafanya kazi za kiuandishi wanayo fursa ya kufikia vigezo vya kuitwa waandishi wa habari kwa mujibu wa kanuni hizo ambazo tayari zimeanza kufanya kazi.” Alifafanua.
Aidha Dkt. Abbasi amesema, Sheria hii ya sasa inatoa fursa kwa chombo cha habari kuomba radhi na kuchapisha habari ambazo zina makosa kwa nia ya kuzisahihisha, na swala hilo likakubaliwa kisheria na halitapelekwa mahakamani chini ya kifungu cha 40 cha sheria ya Huduma za vyombo vya habari.
Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Meneja Uendeshaji wa BoT tawi la Zanzibar, Bi. Graceana Bemeye aliwashukuru waandishi hao kwa ushiriki wao uliotukuka. "Niwahakikishie kuwa BoT, inatambua umuhimu wa waandishi wa habari katika shughuli zake za kila siku, hivyo tutaendelea kutoa mafunzo haya ili kujenga uwezo wa waandishi kuandika kwa usahihi habari zinazohusu BoT kwa manufaa ya taifa.Aidha Kaimu Meneja Uhusuiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Bi. Vicky Msina, alisema mafunzo yaliyotolewa na BoT kwa waandishi hao wa habari ni moja ya majukumu ya BoT katika kuelimisha umma na kwamba mafunzo hayo yalijumuisha waandishi wa habari kutoka Tanzania bara na visiwani.
Mkurugenzi wa Habari nchini Dkt.Hassan Abass akitoa mada ya sheria kwa vyombo vya Habari katika mafunzo ya waandishi wa Habari. |
Baadhi ya waandishi wa Habari wakisikiliza mada katika mafunzo hayo. |