Wednesday, April 5, 2017

WALIMU HANDENI WAMOTISHWA

Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imezipongeza na kutoa zawadi kwa shule kumi za Msingi na   Sekondari moja kwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya  mwaka jana darasa  la saba na kidato cha nne. Zawadi hizo zilitolewa kwenye kilele cha maadhimisho ya juma la elimu yaliyofanyika kiwilaya Wilayani Handeni kwenye shule ya Msingi Kabuku nje.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Handeni   ambaye pia alikuwa mgeni rasmi Mh. Godwin Gondwe aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri wanazofanya na wanazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.

“elimu ni ufunguo wa maisha na kwamba Handeni hakuna mtoto mjinga, wazazi na walezi himizeni  watoto kutumia fursa ya Elimu bure inayotolewa na na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli” Alisema.

Aidha ameeleza pia,atahakikisha fedha zinazohusu madai ya walimu  zinapofika  Halmashauri zinawafikia walengwa kwa wakati uliopangwa. Aliwataka wakuu wa shule na waratibu wa elimu kusimamia haki ya msingi ya wanafunzi kupata elimu

Wakati huohuo amepiga marufuku watoto walio na umri wa kwenda shule kuchunga mifugo hasa kwa siku za shule baada ya kubainika watoto wengi wa jamii ya wafugaji wanatumiwa kuchunga mifugo badala ya kwenda shule. Amewaonya wazazi na jamii ya wafugaji ambao wanakwamisha watoto kupata haki yao ya msingi ya kupata elimu na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume. Amewaeleza pia wazazi ambao wana watoto waliovuka umri wa kwenda shule kupelekwa kwa utaratibu wa MEMKWA.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Bw. William Makufwe ,amesema kuwa  kukosekana kwa chakula cha kutosha shuleni,utoro uliokithiri kwa baadhi ya wanafunzi,kutokuwajibika kwa baadhi ya walimu na wazazi pamoja na upungufu wa walimu kunasababisha kwa kiwango kikubwa kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi.

Ameagiza shule ambazo mpaka sasa hazina chakula kuhakikisha wanawapa wanafunzi  chakula hadi kufikia mwezi mmoja na kusimamia mazao ya mihogo waliyopanda ili mazao hayo yaweze kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni  na kuongeza kiwango cha uelewa kwa wanafunzi. Ametoa mwezi mmoja hadi kufikia 4/5/2017 kwa maafisa watendaji wa kata,vjiji,walimu wakuu,wakuu wa shule na waratibu Elimu wa Kata kuhakikisha kuwa watoto wanapata chakula cha mchana shuleni

Shule zilizopata zawadi na pongezi ni Tewe iliyokuwa ya sita kimkoa na kuzawadiwa Tsh. 200,000/=., Chang’ombe Tsh. 150,000/=, Mkumba Tsh 100,000/=, Mzundu Tsh. 82,000/=, Kwaragulu , Mbwewe, Kwamdani, Kwedikwazu Magharibi, Kwedikwazu Mashariki na chogo ambazo zote zilipata Tsh 78,000/=. Mazingara sekondari imepata zawadi Tsh.100000/
6 Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akizungumza wakati wa Hafla hiyo

4.Mwanafunzi wa shule ya sekondari kabuku akielezea mifumo ya kibaiolojia Kwa viongozi.

 Mwalimu na wanafunzi wakisherehesha Hafla hiyo.

2.Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe na Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe wakisomewa namba na wanafunzi wa shule ya awali kabuku nje.

Caption 1. Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe akikabidhi zawadi kwa mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Tewe iliyokuwa ya kwanza kiwilaya na ya sita kimkoa.

5.Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh Godwin Gondwe wakatikati na Mkurugenzi Mtendaji Bw William Makufwe wa mwisho kulia na kaimu afisa Elimu Msingi Bw Fikeni senzige wakikagua gwaride la wanafunzi wa kabuku.