Friday, April 28, 2017

Watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi wafutwa utumishi


Rais Magufuli leo amepokea ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma zoezi lililofanywa na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini pia taasisi nyingine za serikali.
Ripoti hiyo imekabidhiwa kwake na Waziri Angella Kairuki ambaye ndiye mwenye dhamana na watumishi wa umma, lakini kabla ya kuikabdhi alitoa taarifa za mchakato mzima ulivyokwenda.
Katika taarifa ya Waziri Kairuki amesema, matokeo ya uhakiki wa vyeti yamegawanyika katika makundi manne. Kundi la kwanza ni watumishi wenye vyeti halali. Kwa mujibu wa waziri huyo watumishi asilimia 94 ya wale wote waliohakikiwa walikuwa na vyeti halali.
Kundi la pili ni lile la watumishi wenye vyeti vya kughushi. Kwa mujibu wa Waziri Angella Kairuki, jumla ya watumishi 9,932 kati ya watumishi wote waliohakikiwa walikutwa na vyeti vya kughushi. Kundi la tatu ni la watumishi wenye vyeti vyenye utata. Kwa taarifa ya Waziri Kairuki, jumla ya vyeti 1,538 vilikutwa na utata ambapo vinatumika na mtu zaidi ya mmoja. Watumishi 3,076 walibainika kutumia vyeti hivyo 1,538.
Aidha, kundi la nne na la mwisho, ni watumishi waliowasilisha vyeti pungufu. Wakati wa uhakiki kuna baadhi ya watumishi waliwasilisha vyeti pungufu na hivyo kufanya uhakiki wao kutokukamilika. Waziri Kairuki amesema kuwa watumishi wengi hawakuwasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne na sita.
Baada ya taarifa hiyo, Waziri Kairuki alikabidhi ripoti kwa Rais Magufuli na kisha Rais akamapata nafasi ya kuzungumza na kutolea maamuzi baadhi ya mambo yaliyowasilishwa kutoka kwenye ripoti hiyo.
Akizungumza kuhusu watumishi 9,932 wenye vyeti vya kughushi, Rais Magufuli amemuagiza Waziri Angella Kairuki pamoja na Waziri Mkuu na Wizara ya Fedha kuhakikisha watumishi hawa wanaondoka kwenye ajira haraka iwezekanavyo. Pia, Rais Magufuli amesema kuwa kwa wale watakaoondoka kwa hiari yao hadi Mei 15 mwaka huu wasishtakiwe, lakini wale watakaojikuta wana kiburi wakamatwe na kufikishwa mahakamani ambapo adhabu ni kifungo cha hadi miaka 7.
Aidha, ameiambia Wizara ya Fedha kuwaondoka katika mfumo wa malipo watumishi hao, na mshahara wa mwezi Aprili wasilipwe. Wakati huo Rais ameagiza kutangzwa kwa nafasi za kazi kwa hao walioondolewa madarakani ili zijumlishwe na 52,456 zitakazotolewa katika mwaka wa fedha 2017/18.
Kuhusu watumishi wenye vyeti vyenye utata, Rais Dkt Magufuli ameagiza kuwa, watumishi 3,076 wanaotumia vyeti 1,538 wasilipwe mishahara yao hadi hapo mmiliki halali atakapofahamika ni nani. Lakini ametoa muda kwa mtumishi anayetumia cheti cha mtu mwingine kujisalimisha mwenyewe kwani atapatikana.
Akitolea maamuzi watumishi ambao hawakuleta vyeti vyote, Rais Magufuli ameagiza hawa waendelee kulipwa lakini uchunguzi zaidi ufanyike kwa sababu wengine hawakupeleka vyeti vya kidato cha sita kwa sababu hawakupitia kidato cha sita. Hivyo ni vyema uchunguzi wa kina ukafanyika ili asiwepo atakayeonewa.

WaAkizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Waziri wa Elimu, Prof. Ndalichako aliwasihi wanafunzi kuwa, kama kuna yeyote anajijua anatumia vyeti feki basi ajisalimishe mwenyewe maana atakamatwa tu hata akishamaliza chuo.