Friday, May 12, 2017
DC: Wauguzi Timizeni Wajibu Wenu
Wauguzi wilayani Kishapu wamepongezwa kwa kazi nzuri na kutakiwa kuendelea kuipenda kazi yao kuchapa kazi katika mazingira yoyote waliopo kwani wao ni chachu ya afya katika jamii.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba wakati kwenye kilele cha Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya DK. Jakaya Kikwete.
Talaba ambaye aliwaongoza wauguzi hao na watumishi wa halmashauri kutoa misaada na kufariji wagonjwa hospitalini hapo aliwapongeza kwa huduma nzuri kwa wagonjwa.
Alisema kuwa bila ya wauguzi afya haijakamilika na kuwa uuguzi ni zaidi ya wito na ni huduma inayohitaji upendo na huruma kwa wale unaowahudumia.
“Kama huna upendo na ukarimu basi wewe siyo muuguzi na ukionesha ukarimu na upendo ndiyo mwanzo wa kupona kwa mgonjwa ukifika tu pale mgonjwa anapona hata kabla hujampa dawa,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wauguzi waendelee kuwa na ushirikiano baina yao huku akiwapongeza kwa mafanikio katika sekta ya afya pamoja na kuwa wana changamoto ya mazingira ya kazi.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba kuendelea kutimiza wajibu na kuzingatia viapo vyao vya uuguzi na kanuni za utumishi huku akionya kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za kazi na hivyo kutengeneza migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande wake, Kaimu Muuguzi Mkuu Hospitali ya wilaya hiyo ya Dk. Jakaya Kikwete, Rehema Jumanne akisoma risala alitaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni mafunzo kazini.
Alisema mafunzo hayo yamesaidia wauguzi kuboresha huduma za jamii zikiwemo uzazi wa mpango, huduma za dharura kwa wajawazito na kusaidia wachanga kupumua.
Pia alitaja mafanikio mengine ni kuendeleza wauguzi katika ngazi za juu za elimu na hivyo kutoa huduma kwa kiwango cha juu pamoja na kutoa huduma bora tofauti na mazingira yao.
Hata hivyo alisema kuna changamoto ya uhaba wa watumishi hiyo husababisha kutokuwepo kwa uwiano sawia wa watumishi katika kutoa huduma katika vituo vya afya na zahanati mbalimbali katika wilaya hiyo.
Siku ya Wauguzi Duniani huadhimisha kila Mei 12 ikiwa ni kumuenzi muuguzi mwanzilishi Florance Nightingale aliyoanzisha mwaka 1844 ambapo kaulimbiu ni Wauguzi, mbiu ya kuyafikia malengo endelevu ya millennia.