Friday, May 12, 2017
Kishapu Yazindua Mashindano ya UMISSETA
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imezindua mashindano ya Michezo ya Sekondari Tanzania (UMISETA) kwa mwaka 2017 kitarafa katika viwanja vya shule ya sekondari Shinyanga.
Mashindano hayo yamehusisha mpira wa miguu, netiboli, kikapu, wavu na riadha ambapo yatashirikisha shule za tarafa mbalimbali wilayani humo ambapo washindi watashindanishwa kupata timu za wilaya.
Akizungumza na wachezaji kutoka shule za Shinyanga sekondari, Maganzo Songwa, Mwadui ufundi, Idukilo na Mwadui Lutheran kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji, Ofisa elimu sekondari, Paul Kasanda aliwataka kuwa wamoja.
Alisema pamoja na kuwa wachezaji hao wanatoka shule mbalimbali wilayani humo wanapaswa kushirikiana na kupata ushindi pindi watakapocheza na wilaya zingine kutafuta wawakilishi ngazi ya taifa.
Kasanda aliongeza kwa kusema kuwa michezo ni upendo, furaha, huleta furaha na pia huweza hata kutoa ajira kama zingine endapo wachezaji watajituma vizuri wataweza kufika mbali.
“Pamoja na kuwa ninyi ni wamoja mnatoka wilaya moja lakini tunataka mtuoneshe ufundi wenu, vipaji na ushindani ili tupate timu bora zitakazoshindana na wilaya zingine,” alisema Kasanda.
Mashindano ya UMISETA kiwilaya yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 21 ambapo kimkoa ni Mei 22 hadi Juni 5 wakati kitaifa ni Juni 6 hadi 15 mwaka huu.