Thursday, May 11, 2017
Nape Nnauye akionya Chama cha Mapinduzi(CCM)
Mbunge wa Mtama na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amekionya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba kisipotekeleza ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wanaweza wasiaminiwe tena katika uchaguzi ujao.
Nape ameyasema hayo kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter ambapo ameandika “Tuliwaahidi na huu ndio mkataba kati ya CCM na Wananchi! Tusipoutekeleza hatutaaminika!”
Tuliwaahidi na huu ndio mkataba kati ya CCM na Wananchi! Tusipoutekeleza hatutaaminika! pic.twitter.com/bAfCiJhhag
— Nape Moses Nnauye (@Nnauye_Nape) May 11, 2017
Tangu alipovuliwa uwaziri, Nape amekuwa akichapisha picha mbalimbali za shughuli alizokuwa akizifanya nchi nzima kuimarisha chama ili wananchi waweze kukiamini kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.
Aprili 4 mwaka huu, Nape aliuliza swali lake la kwanza bungeni baada ya kuvuliwa uwaziri ambapo alilielekeza katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akitaka serikali iwe inahakikisha kuwa imekamilisha mipango yake ndipo iweke X kwenye nyumba za wananchi zitakazobomolewa na si kuziwekea alama hiyo halafu hakuna kinachoendelea, jambo linaloathiri maendeleo.
Aidha, akiwa bugeni, Nape Nnauye ameijia juu serikali kuhusu kupunguzwa kwa bajeti ya maji kutoka zaidi ya bilioni 900 kwa mwaka 2016/17 hadi kufikia bilioni 672.2 kwa mwaka 2017/18 ikiwa ni punguzo la asilimia 30.
Akichangia hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Nnauye alisema mabadiliko yanayofanywa na Rais Magufuli hayatakuwa na manufaa kama huduma za jamii hazitoboreshwa, huku akishauri bajeti hiyo kuongezwa.
Mbali na Nape, wabunge wengine waliopata nafasi ya kuchangia hotuba hiyo akiwemo, Zitto Kabwe, Mussa Mbarouk, Suleiman Bungara, Tunza Malapo na Dk. Mary Nagu waliunga mkono hoja ya bajeti ya wizara hiyo kuongezwa kwani maji ni tatizo linalowakumba wanachi wengi nchini.
Nape kwa upande wake amekuwa akisema kuwa sasa ni wakati wa kiwatumiakia wananchi wa Mtama walioumuamini na waliokiamini chama chake, kwani asipofanya hivyo kwa kutekeleza ahadi zake, hatoaminiwa tena.