Monday, November 5, 2018

YALIYOJIRI WAKATI MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DKT. HASSAN ABBASI AKITOA TAARIFA YA MAMBO MUHIMU YALIYOTEKELEZWA NA SERIKALI YA AWAMU TANO NDANI YA MIAKA MITATU*

*

#Leo Novemba 5, 2018 ni miaka mitatu ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano; ni zaidi kidogo ya nusu ya muhula wa miaka mitano ya awali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa madarakani.

#Rais Dkt.John Magufuli anawashukuru Watanzania wote ambao wameendelea kuiunga mkono Serikali yake kwa namna mbalimbali ikiwemo kutimiza wajibu wao kama vile kulipa kodi, kuchapakazi kwa bidii na kuishi kwa maadili.

#Ahadi kuu ya Rais Magufuli  katika miaka ijayo kwa watanzania wote ni kuwa yeye binafsi na Serikali yake nzima wataendeleza mageuzi ya kweli ambayo leo hapa tutaangalia baadhi ya mafanikio yake.

#Rais Magufuli Anawaomba muendelee kumuombea yeye binafsi na Serikali yake, kudumisha, amani na kila mtu awe na upendo na uzalendo kwa Taifa lake.

#Miaka mitatu leo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi wa dunia na hata ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania chini ya Rais Magufuli imeendelea kuwa na uchumi unaoendelea kukua kwa kasi nzuri.

#Katika mwaka 2017/18 uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 na kuongoza katika nchi zote za Afrika Mashariki lakini ukiingia katika rekodi ya kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kimataifa.

#Katika miaka hii mitatu Rais Magufuli amethubutu kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza kasi ya kukusanya kodi na hivyo kuongeza mapato ya kodi ya Serikali kutoka wastani wa TZS Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa TZS Trilioni 1.3 kwa mwezi.

#Kutokana na ufuatiliaji, ubunifu, uwekezaji wa Serikali ya Rais Magufuli mashirika mengi ya aina hiyo sasa yameanza kuamka kuwa na ufanisi, kuongeza mapato na mengine kutengeneza faida. Kwa minajali ya muda nitatoa mifano michache kwa Mashirika kama TTCL, TRC, DAWASA na Bandari.

#Rais Magufuli alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita aliahidi kurejesha azma ya tangu wakati wa Baba wa Taifa ya kujenga Nchi ya Viwanda. Katika kipindi hiki viwanda 3,306 viliandikishwa, vinaendelea kujengwa na baadhi vimekamilika na vinatoa bidhaa mbalimbali. Kati ya hivyo 251 ni vikubwa na vya kati ni 173.

#Licha ya mchango kwa Pato la Taifa, masoko na jamii kupata malighafi, ujenzi na kuanza kazi kwa baadhi ya viwanda vipya, tayari kumeanza kusaidia kuwapatia ajira Watanzania. Takwimu za mpaka Juni 30, 2018 zinaonesha kuwa sekta ya uzalishaji viwandani imefikisha ajira 280,899 kutoka ajira 254,785 mwaka 2015.

#Tayari mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi 5.5 mwaka 2017. Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Viwanda ilikua kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 7.1 mwaka 2017/18.

#Viwanda katika miaka hii mitatu vimeongeza ajira kwa zaidi ya Watanzania 26,000 huku ajira nyingine zaidi ya 100,000 zikitarajiwa kuongezeka kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali ipatayo 905 iliyosajiliwa kupitia TIC mingi ikiwa viwanda, majengo, kilimo.

# Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi kwa, pamoja na mambo mengine, kutimiza Ahadi yake ya kuunda Mahakama ya Mafisadi.

#Mahakama ya Mafisadi (Makosa ya Uhujumu Uchumi) ilianza kazi rasmi Julai, 2017. Mpaka sasa kesi mpya 41 zilifunguliwakuna na maombi ya dhamana 346 yamewasilishwa katika Mahakama hii kati ya 2007 na 2018.

#Kwa upande wa PCCB nayo imeendelea kwa kasi kuzuia na kupambana na rushwa ambapo kesi mpya 495 zilifunguliwa kati ya mwaka 2016 na 2017 ambapo asilimia 60.14%  walifungwa.

#Takukuru imeokoa TZS Bilioni 70.34 zilizokuwa zilipwe kifisadi na imezuia Bilioni 42.16 na Euro 4.3m mpaka kesi ziishe.

#Baada ya mafanikio ya Serikali kuleta ndege nne mpya zinazoendelea kuleta mageuzi katika usafiri wa anga nchini, abiria wanaotumia ndege za ATCL wameongezeka kutoka takribani abiria 4,000 kwa mwezi hadi abiria 30,000 kwa mwezi.

#Tunaleta AIR BUS  mbili zenye uwezo wa watu 132+ zinawasili nchini Disemba, 2018 na BOEING DREAMLINER ya 2: Hii inakuja nchini Oktoba mwaka 2019.

#Katika kipindi hiki, Serikali imeanza au inajiandaa kutekeleza miradi mikubwa na ya kihistoria kwa maendeleo ya Taifa ikiwemo utandikaji wa reli ya kisas( Standard Guage).

#Serikali imetekeleza miradi muhimu kwa maisha ya watu katika masuala ya Afya, Elimu na Nishati.

#Serikali imeokoa mabilioni ya fedha za wananchi kwa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme wa gesi badala ya kutegemea mitamgo ya mafuta. Miradi ya Kinyerezi I-Extension (megawati 185) na Kinyerezi II (megawati 240+) inaelekea kukamilika. Tayari Kinyerezi II peke yake imeshaingiza megawati zaidi ya 200 kwenye gridi ya Taifa.

#Serikali imeongeza bajeti ya fedha za ndani ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoka Shilingi bilioni 290.2 mwaka 2014/15 hadi Shilingi bilioni 375.38 mwaka 2018/19 na na kazi ya Awamu ya Tatu ya Usambazaji Umeme Vijijini imeanza na inaendelea.

#Serikali imewekeza katika sekta ya afya ikiwemo kujenga Vituo vya Afya vya Kata 210 na kukarabati vingine vingi kufikisha idadi ya vituo vinavyotoa huduma hadi mwaka huu kuwa 7,746 kutoka vituo 7,014 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 10.4. Vituo hivi pia vina wodi za kina mama na vifaa vya kisasa. Aidha, ajira zaidi ya 6,000 za kada ya afya zimetolewa.

#Katika miaka mitatu Zahanati zimeongezeka kutoka 6,143 mwaka 2015 hadi 6,646 mwaka huu (Ongezeko la zahanati 503) ambapo baadhi zilijengwa na zingine kukarabatiwa sawa na ongezeko la asilimia 8.1.

#Kazi kubwa imefanyika kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa ikiwemo kununua CT-Scan, MRI, Digital scanners na kuimarisha tiba za kibingwa kama moyo, kupandikiza ini na oparesheni za mifupa, mgongo na masikio (Cochler inplant).  Vifaa hivi vimepunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje kutoka wastani wa 553 mwaka 2015/16 hadi 103 mwaka wa fedha uliopita.

#Kutokana na kuimarika tiba hizi za kibingwa tumeshapokea wagonjwa kutoka nchi za: Komoro, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, DRC, Zambia na wataalam wa nje zinaleta wagonjwa wao kutibiwa Tanzania).

#Serikali imeendeleza jitihada za kuongeza huduma ya maji kwa lengo la kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini. Miradi mikubwa na midogo inaendelea kote nchini.

#Miradi 1,571 yenye jumla vituo vya maji 126,610 imekamilika na baadhi inakamilika, na itakapokamilika yote iliyobaki itafikisha uwezo wa kuhudumia jumla ya watu milioni 31.65 sawa na asilimia 81 ya wakazi waishio vijijini.

#Katika Elimu ya juu Serikali ya Awamu ya Tano imemaliza  migomo isiyo ya lazima kwani si tu Bajeti Elimu ya Juu imepanda hadi TZS Bilioni 427.5 mwaka huu kutoka Bilioni 348 mwaka 2015, fedha hizo sasa zinatoka mapema (Mfano: Bilioni 137 zilishatolewa tangu Septemba mwaka huu kusubiri wanafunzi wapya kupewa fedha za siku 60 za kwanza).

#Katika jitihada za Serikali kuvutia wanafunzi wengi zaidi kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati, si kuimarisha masomo ya sanaa pekee, Serikali inatekeleza mkakati wa kukamilisha maabara 3 za Sayansi katika kila shule.  Kwa sasa shule za Serikali zenye maabara ni 2,141 kati ya 3,614.

#Ukuta wa Mererani umewezesha Serikali kupata mapato kutoka Milioni 71 hadi kufika Bilioni 1.2 .

#Katika miaka hii mitatu licha ya matukio ya hapa na pale, bado Tanzania, imesimama kama moja ya visiwa vya amani duniani na Tanzania.

#Rais Magufuli amesimamia misingi ya Taifa ambapo Watanzania leo tuko huru kuamua mambo yetu kama Taifa, safari ya kujitegemea imeanza na hata Mataifa makubwa na madogo yanafahamu kuna mtu huyu anaitwa JOHN POMBE MAGUFULI na ana azma gani kwa Taifa lake. Miradi aliyoianzisha kwa fedha za ndani ni utekelezaji wa azma hiyo.

#Kama nchi tunapaswa kuendelea kupambana na wanamaslahi mbalimbali ambao hawafurahishwi na mageuzi haya, lazima tuungane kuwapinga na kuendelea kuwapa moyo viongozi wetu.

#Mataifa yaliyofanikiwa yamepita katika vipindi vya mageuzi. Nasi tunapaswa kupitia mkondo huo huo. Mataifa kama China, Malaysia, Indonesia n.k tulikuwa nao karibu sawa leo wako mbali hivyo Tanzania itajengwa na watu wenye kuchapakazi, kujituma, kulipa kodi na kuwa watiifu.

*Imetayarishwa na Idara ya habari- MAELEZO*