Saturday, April 22, 2017

JUKWAA LA UWEZESHAJI KIUCHUMI WANAWAKE LAZINDULIWA

Halmashauri ya Wilaya ya Handeni imezindua jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa wanawake wa Wilaya ya Handeni  kwenye ukumbi wa maount Ilulu uliopo Kabuku mjini lenye ujumbe wa “Wezesha wanawake kiuchumi ili kujenga uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda”.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni Bw.John Mahali akitoa hotuba ya uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji wanawake Kiuchumi

Kiongozi wa Jukwaa la wanawake akikabidhiwa Katiba  ya kikundi

Viongozi wilayani Handeni wakikagua na kuona kazi  za wanawake wajasiriamali baada ya uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi

Jukwaa hili linalengo la kuwakutanisha wanawake pamoja na kujadili fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi katika Wilaya ya Handeni.

 Akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni  Bw. John Mahali aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh. Godwin Gondwe alisema kuwa jukwaa la wanawake hilo  litasaidia  kuongeza uelewa kwa wanawake katika upatikanaji  wa mitaji , sheria za nchi katika masuala ya kiuchumi na jinsi ya kujitegemea.

Aliongeza kuwa wanawake wamekuwa hawapati fursa za kutosha za kiuchumi hapa Nchini hata na duniani kote kutokana na kutokuwa na usawa katika fursa , uwezo wa kupata mitaji.

“jukwaaa litasaidia kuondoa matabaka na sheri ambazo zitasaidia kupunguza ubaguzi wa kiuchumi kwa wanawake, ambalo ni jambo la muhimu sana katika kuleta maendeleo ya usawa katika pato la Taifa, jamii na familia” alisema Bw. John.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Handeni Bw. William Makufwe alisema kuwa  jukwaa hili litafanya kazi ya kutambua shughuli za kijasiliamari katika kutoa elimu kuhusu upatikanaji wa mitaji, kusajili biashara, kuwezesha kiuchumi na kutafuta masoko.

Aidha, alisema katika suala la utoaji mikopo vikundi vitakavyopewa kipaumbele ni vile viliyojidhatiti kwa kusajiliwa, vyenye utawala unaoeleweka, miradi inayoonekana na zenye hesabu za kifedha zinazoweza kukaguliwa na kukosolewa inapobidi.

Uzinduzi huo ulipambwa na maonesho ya bidhaa za kijasiliamari ya vikundi mbalimbali kutoka kata mbalimbali. Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga itaratibu shughuli zote za uchumi kwenye Wilaya zote ndani ya Mkoa na kuhakikisha kunakuwa na majukwaa ya Wilaya/Halmashauri zote ambayo yatafanya  vikao vyake kila baada ya miezi sita (6).