Wednesday, March 29, 2017

KUMBE MFUMO SI LOLOTE



WATU fulani wakati tunaelekea kwenye uchaguzi wa 2015 na hata baada ya uchaguzi walikuwa wanasema Magufuli yuko vizuri lakini tatizo lililopo ni MFUMO.

Wakasema JPM ndie kiongozi sahihi wa Tanzania kwa wakati huu lakini tatizo anatoka CCM.

Wengine wakasema ana uwezo na nia ya dhati ya kuitendea mema nchi hii lakini tatizo ni MFUMO.

JPM amekua Rais tayari na mwelekeo wake umeonekana kuanzia udhibiti wa mapato, udhibiti wa matumizi holela ya Serikali, udhibiti wa nidhamu ya watumishi, uendelezaji na ujenzi wa miundo mbinu ya bara bara, reli,bandari na majengo mbali mbali na utoaji wa huduma za jamii.

Katika kuchukua hatua hizo ambazo ni kwa manufaa ya kizazi cha leo na vizazi vijavyo, WAMEIBUKA wale wale waliokuwa wakidai JPM atakwamishwa na MFUMO na sasa wanapinga kila kitu.

Bahati mbaya sana wanapinga kila jambo hata yanayowanufaisha wao na vizazi vyao, wanatetea kila dhambi hata dhambi ambazo hapo mwanzo walilia hadharani kuwa wanazichukia.

Sasa hawataji tena MFUMO, lakini baada ya JPM kuwa Rais nimegundua yafuatayo:

Kumbe MFUMO uliokuwa unalalamikiwa sio CCM kama umma ulivyoaminishwa hapo awali wala sio Serikali kama walivyojaraibu kutuambia.

MFUMO ni watu, tena watu kutoka kada zote ambao wana maslahi katika sekta mbali mbali na walizoea kila uchao kutengeneza  namna ya kuwezesha mambo yao na kulinda maslahi yao.

Wana MFUMO huo kumbe ni wale waliozoea kujilimbikizia mali, kuendekeza rushwa, uporaji wa mali za umma, utendaji wa kimazoea na kwa ujumla kuishi kwa staili ya "kupiga dili."

Tofauti na tulivyoaminishwa kuhusu MFUMO kumbe MFUMO wenyewe uliokuwa unaikwaza nchi unahusisha wananchama wengi wakiwemo waliomo katika baadhi ya maeneo Serikalini, katika siasa, makanisa, biashara, vyombo vya habari na sekta nyingine.

 Waswahili wanasema "rusha jiwe kichakani,utawajua waliomo" sasa mageuzi makubwa anayoyafanya Rais Magufuli yamewaibua wanamaslahi wa MFUMO TATA.

Rais Magufuli katika utekelezaji wake wa majukumu,utekelezaji unaohusu kumkomboa mtanzania masikini na kuijenga Tanzania mpya itayokuwa kioo kwa Afrika na dunia nzima, amegusa MFUMO na akaenda mbali zaidi kwa kuugusa na MFUMO TATA.

Amerusha jiwe kichakani na waliofichama humo tumeanza kuwajua, na ni rahisi sana kuwajua waliokuwa wakitukwaza tusiendelee.

Sasa tunawaona wakitimua mbio, tumesikia vilio vyao wakitetea rushwa waliyoipinga awali, wakililia wanaotumbuliwa wakati awali walikerwa na watu kutochukuliwa hatua.

Tena kuna mmoja alitaka kufika hatua ya kuwakusanya watu waandamane kuzuia mchanga wa dhahabu usisafirishwe nje eti leo marufuku imewekwa nasikia anahaha huku na kule kutaka mchanga uruhusiwe tena kwenda nje. Jiwe limefika kichakani


Kumbe ule mfumo sio Serikali, CCM wala siasa au biashara bali ni  watu ambao waliifanya CCM kuwa kichaka, Serikali kuwa pango lao na siasa au biashara kama handaki la kuficha maovu na maslahi yao.

Hiyo ndiyo kazi ya MFUMO, MUNGU ametupa Rais Magufuli ili tuujue ukweli, tuujue huo unaoitwa MFUMO,tujitambue na tutambuane na kweli tumeanza kutambuana.

Viva JPM endelea kurusha mawe kizani, watatoka wenyewe.

                                         "HAPA KAZI TU "
Ukumbi wa mikutano wa Kikwete,mahali ambapo mikutano na vikao mbalimbali vya maamuzi vya Chama cha Mapinduzi hufanyika