Akizungumza wakati wa kusaini kwa mkataba wa msaada huo, Balozi wa Japani hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida alisema kwamba msaada huo ni matokeo ya Ombi la Mhe Cosato Chumi Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini aliloliwasilisha Ubalozini mwaka uliopita.
Aidha Mhe Balozi Yoshida alimpongeza Mbunge huyo kwa ushirikiano alioutoa hasa katika kufuatilia katika ngazi mbalimbali za serikali ikiwemo Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata ridhaa ya kusaini mkataba wa msaada huo.
Pamoja na msaada huo, Serikali ya Japan kupitia Ubalozi wake hapa nchini, umetoa msaada kwa Halmashauri za Bukoba, Temeke na Chuo cha Ufundi Yombo.
Halmashauri ya Bukoba imepewa msaada wa USD 108,025 (Tsh (238m) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwenye shule za Msingi za Nyakato na Kashozi ambazo ziliathiriwa na tetemeko la ardhi.
Kwa upande wa Temeke wamepokea msaada wa USD 137,837 (Tsh 274m) kwa ajili ya kuboresha Jengo la Huduma ya dharura kwenye Hospital ya Rufaa ya Temeke.
Chuo Ufundi Yombo wamepokea msaada wa USD 64,499(Tsh 130m) kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vya madarasa ya wanafunzi wenye ulemavu.
Jumla ya USD 408,496 (Tsh 900m) zimetolewa katika misaada hiyo inayolenga kuwasaidia wananchi ngazi za chini yaani Grant Assistance for Grassroots Human Security Projects .
Akizungumza Mara baada ya kusainiwa kwa mikataba ya misaada hiyo, Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi, alimshukuru Balozi Yoshida na Serikali ya Japan kwa kuendelea kufadhili miradi hasa inayolenga kuwafikia watu wa chini.
Aidha Chumi alimshukuru Wizara ya Fedha kwa kuridhia kusainiwa kwa mikataba ya misaada hiyo kabla ya kumalizika kwa mwaka wa Fedha wa Japani Machi 31. 'Namshukuru Sana Mhe Dkt Philip Mpango na watendaji wake kwa jinsi ambavyo walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa taratibu zote za kisheria na kikanuni zinatimizwa kwa wakati ili mikataba hii iweze kusainiwa siku ya leo'
'Pamoja na misaada mikubwa kupitia ushirikiano baina ya nchi hizi mbili yaani bilateral cooperation , bado Japan imeendelea kutoa na kufadhili miradi inayotekelezwa katika ngazi za chini kabisa, hili ni jambo jema na tunaopokea Fedha hizi tuzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa' Alisema Chumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Bi Saada Mwaruka alisema kuwa msaada huo ni ukombozi kwa watu wa Mafinga na Mufindi kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba Hospital hiyo inahudumia Wilaya ya Mufindi na hata Wilaya za jirani kama Mbalari na Iringa Vijijini.
Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia kuanzia mwaka 2011 jumla USD 6.7m (Tsh 15bilioni) zimetolewa na Serikali ya Japan maalum kwa ajili ya kufadhili jumla ya miradi sitini (60) ya Afya, Elimu na Maji. Miradi hiyo imetekelezwa katika ngazi za Halmashauri.
Mari wa Japani nchini Tanzania akitoa Maelezo kabla ya kusaini mkataba. |