TOVUTI ZA SERIKALI KUBORESHA USIMAMIZI NA USHIRIKISHWAJI WA WANANCHI
Sekretarieti za mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Halmashauri zake 185,zimezindua tovuti zake mpya katika uzinduzi wa kitaifa,tukio hili limefanyika mkoani Dodoma mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais -Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa,Mh George Simbachawene.Uzinduzi huu wa kitaifa umeshirikisha mawaziri na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma. Angela Kairuki,Waziri wa Habari,Utamaduni na Michezo,Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe,na Mkurugenzi wa USAID/Tanzania,Tim Donnay,pia walihudhuria.
Kwa upande wa uzinduzi wa tovuti kwa Kanda ya kisini ulifanywa na mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe.Evodius Mmande kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mtwara.
Katika hotuba yake ya uzinduzi alisisitiza kwa maafisa habari kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa mafunzo na sheria za habari nchini.Ikiwa ni pamoja na kutoa habari zilizochambuliwa na kufafanuliwa vizuri ili ujumbe uwafikie wananchi kwa wakati na zisiwe na madhara kwa wananchi.
Mhe.Mmande amewataka wakuu wa taasisi kuondokana na urasimu wa utoaji taarifa kwa maafisa habari kwani utoaji taarifa kwa umma ni suala la kisheria halihitaji urasimu.
Aidha amesema kuhusu upungufu wa watumishi wa kada za Tehama na Habari katika halmashauri na sekretarieti za mikoa ni changamoto inayoweza kupelekea tovuti hizi kutofanya kazi zake ipasavyo.
Ametoa Rai kwa TAMISEMI na Utumishi kuhakikisha kada hizi zinapata watumishi kwani ni muda muafaka kuwa na watumishi hawa.
Mwisho,mgeni rasmi aliishukuru serikali ya Marekani kupitia shirika lake la misaada la USAID,PS3,TAMISEMI,EGA na washiriki wote wa mafunzo na kuwataka washiriki kuyatekeleza kwa vitendo mafunzo waliyoyapata,na akazindua tovuti 26 za mikoa ya Ruvuma,Lindi na Mtwara.