Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)
wilayani Bagamoyo imekagua jumla ya miradi ya maendeleo 20 katika kata 12 za halmashauri ya wilaya ya
Chalinze hivi karibuni, miradi hiyo ni afya 10, elimu 5,viwanda 2,ofisi za
watendaji 2 na soko 1,ikiwa ni moja ya kazi ya kamati hiyo kukagua na kuona
utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2015-2020 inayotekelezwa kwa sasa
nchini kote.
Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo ilikagua na kuona shughuli katika kiwanda cha vigae cha Twyford LTD kilichopo katika kijiji cha Pingi kata ya Pera katika halmashauri ya Chalinze |
Kiwanda cha Vigae katika halmashauri ya Chalinze |
Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo |
Katika ziara hiyo iliyolenga kufuatilia kwa kina utekelezaji
wa ilani ya uchaguzi ya CCM wajumbe walijikita zaidi katika kufuatilia ujenzi
wa miundombinu ya huduma za jamii kwa maana ya afya, elimu,maji,nyumba za
watumishi na kubaini ikama ya watumishi kwa kila kada.Hali kadhalika wajumbe wa
kamati hiyo walitaka kufahamu namna ya utoaji huduma kwa wananchi katika maeneo
waliyokagua ili kuona yaliyoahidiwa katika ilani kama yanatekelezeka kwa
vitendo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Abdul-Rashid
Zahor aliwataka wajumbe kukagua kwa kina na kubaini upungufu katika utekelezaji
wa Ilani ya chama kwa mujibu wa ibara ya ya 49 hadi ya 58 inayo zungumzia sekta
ya huduma za jamii.”Mwaka 2015 tuliahidi kwa wananchi kuboresha huduma za jamii
kwa kuwahakikishia uwepo wa huduma bora za afya,elimu na maji,hivyo hatunabudi
kuzisimamia halmashauri ili zitekeleze kwa wakati na bila kuchelewa kwani 2019
tutasimama kwa wananchi watatuhoji hivyo hatuko tayari kuhojiwa na kukosa
majibu”Zahor alisema.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Kombo Kamote
alifafanua kuwa katika ziara hii tulipanga kukagua miradi katika kata zote 15
za halmashauri ya Chalinze lakini hadi sasa tumeweza kuzifikia kata 12 na
kutembelea miradi ya afya Lugoba,Msoga,Ubenazomozi,Mdaula,Chalinze,Buyuni,Changalikwa,Rupungwi,Kimange
na Miono.Katika ziara hii tumebaini miradi ipo katika hatua mbalimbali ya
ujenzi na inaendelea vizuri kwani mingine ni ya kumalizia na mingine bado iko
katika hatua za msingi.Kwa upande wa sekta ya elimu tumekagua na kuona miradi
katika shule za sekondari Chalinze,Changalikwa,Kimange,Kikaro na shule ya
msingi Mbala.Katika elimu tumekagua ujenzi wa maabara,mabweni,nyumba za
walimu,madarasa na bwalo,kwa upande wa viwanda tumeweza kukagua na kuona jinsi
sekta binafsi zilivyolipokea tamko la serikali kuhusu viwanda kwa kuona
uzalishaji katika kiwanda cha vigae kiitwacho “Twyford LTD”kilichopo katika
kijiji cha Pingo kata ya Pera,kiwanda hiki kinazalisha vigae bora hapa nchini
na kinauza vigae ndani na nje ya nchini kimeweza kutoa ajira kwa watanzania
zaidi ya 900.Vilevile kamati ilitembelea kiwanda cha kuzalisha vinywaji vinavyotokana na matunda mbalimbali
kiitwacho” SAYONA FRUITS”kilichopo katika kijiji cha Msoga kata ya Msoga
kiwanda hiki bado kinaendelea kujengwa na muda si mrefu kitaanza kufanya kazi
na kitatoa ajira kwa wananchi.
Aidha Kamote alibainisha changamoto mbalimbali katika
utekelezaji wa Ilani ikiwa ni pamoja na upungufu wa nyumba za watumishi wa
sekta za afya na elimu,upungufu wa watumishi wa sekta hizi kwa upande wa elimu
kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati hii
imedhihirika baada ya kamati ya siasa kutembelea shule ya sekondari ya
Changalikwa ambayo ilibainika kuwa na mwalimu mmoja wa hisabati kwa shule nzima
kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,Bwana
Deogratius Lukomanya alizipokea changamoto zilizobainika katika ziara hiyo ya
ukaguzi wa utekelezaji wa ilani na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi zile zilizo
ndani ya uwezo wa halmashauri na zile zinazohitaji utekelezaji wa serikali kuu
kuzipeleka panapohusika kwa hatua zaidi.
Katika hitimisho wajumbe wa kamati ya siasa
waliipongeza halmashauri kwa kutekeleza miradi mingi kwa kutumia mapato ya
ndani ni uzalendo wa hali ya juu katika hili na wakaitaka halmashauri kuendelea
kufanyakazi kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ambayo ndiyo dira ya maendeleo kwa
wanachalinze na watanzania kwa ujumla.