Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chalinze,wafanyakazi na wananchi wa mamlaka ya
mji mdogo wa Chalinze wameweza kutekeleza kwa vitendo agizo la Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samiah Suluhu Hassan la kufanya usafi wa
mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi,Wananchi hawa wakiongozwa na
Mkurugenzi Mtendaji ,Bwana Edes Lukoa wamefanya usafi katika kituo cha afya
Chalinze,stendi ya mabasi na soko kuu la Chalinze kwa kuzibua mitaro na kuzoa
taka kwa kutumia lori la kuzolea taka,zoezi hili limefanyika jana Jumamosi kwa
mwitikio wa hali ya juu.
Mkurugenzi wa Hlmashauri ya Chalinze akifanya usafi na wananchi wa Chalinze |
Baada ya shughuli ya usafi wananchi wa chalinze na
wafanyabiashara wa soko la chalinze linalojulika kwa jina la Soko la kwa Mama
Kaguo waliwasilisha maombi yao kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chalinze kutaka wajengewe soko ambalo litakuwa
na mgawanyo mzuri kwa wafanyabiashara
kulingana na bidhaa wanazouza katika soko hilo,kupitia kwa Mjumbe wa
kamati ya usafi ya soko Bwana Abdulratif Gama alisema”Kwa sasa hakueleweki lipi
ni soko kuu na yapi ni masoko madogomadogo kwani hivi sasa tuna masoko
matatu,hapa tulipo kwa Mama Kiguo,kuna soko jingine lijulikanalo kama kwa
Kassim na soko la Shaabani Nguruka ,hivyo tunaomba tuwe na eneo maalum kwa
ajili ya soko”.
Naye Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Lucas Lufunga aliungana
na mawazo ya wakazi wa kata yake ya Bwilingu na kuomba halmashauri iweke
mikakati ya kujenga soko jipya la wilaya kwani hivi sasa Chalinze ni
halmashauri lakini pia ni mamlaka ya mji mdogo ina hitaji kuwekewa mipango
mizuri na endelevu kwa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri Bwana Lukoa aliwataka
wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kufanya usafi kila siku na hususan siku
hii ya usafi kitaifa ambayo imepangwa na serikali kila Jumamosi ya mwisho wa
mwezi iwe ni siku ya usafi,kila mwananchi katika siku hii atekeleze wajibu wake
kuanzia asubuhi saa moja hadi saa nne asubuhi hili ni agizo kila mwananchi
anatakiwa kutii.”Nawakumbusha tena kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi wananchi
mjitokeze kufanya usafi na hili lizingatiwe bila kupuuzwa”
Hata hivyo Bwana Lukoa alitoa ufafanuzi kuhusu uanzishwaji
wa soko la kisasa na kituo cha mabasi kwa hapa Chalinze”Halmashauri inaendelea
na mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko na kituo cha mabasi
hivyo tuvute subira katika hili na tuzingatie usafi kwa hali tuliyo nayo kwa
sasa”.Lukoa alisema.
Usafi katika kituo cha afya cha Chalinze siku ya usafi kitaifa |
Wananchi wa Chalinze wakiwa katika barabara kuu iendayo Dar es salaam wakizibua mitaro katika barabara wakiongozwa na Mkurugenzi wa Chalinze Bwana Edes Lukoa |