Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Alhaj Majid Mwanga amezindua
rasmi kampeni ya chanjo ya kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa watoto wa
kike waliofikia umri wa miaka 14,uzinduzi huo umefanyika jana katika kijiji cha
Kikaro kata ya Miono katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze.Kampeni hizi ni
mkakati wa serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ugonjwa wa saratani ya
mlango wa kizazi ambao umekuwa tishio kwa afya za wanawake hapa nchini na
ulimwenguni kote kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga akizindua zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi |
Shehe Hamis Nasoro akichangia jambo katika uzinduzi wa |
Wanafunzi wa shule ya sekondari Kikaro |
Shehe akihamasisha zoezi la chanjo |
Kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo kulitolewa mafunzo kwa
wadau na wahamasishaji wa masuala ya afya ya msingi katika jamii kwa maana ya
wahudumu wa afya,maafisa watendaji wa vijiji na kata,maafisa tarafa,maafisa
maendeleo ya jamii,viongozi mbalimbali wa dini na walimu wa shule za msingi na
sekondari ili wapate ufahamu kuhusu saratani ya mlango wa uzazi,dalili za
maabukizi ya virusi vya “Human Pappiloma Virus”(HPV),dalili za saratani ya
mlango wa kizazi,chanjo ya kukinga Saratani ya mlango wa kizazi,namna
inavyotolewa chanjo na maudhi madogo madogo yanayoweza kutokea baada ya chanjo
kwa watoto.
Katika mafunzo hayo Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya
Dkt.Rahim Hangai aliwataka washiriki kuwa mabalozi katika kufanikisha zoezi
hili muhimu la kitaifa ili kuwanusuru watoto wa kike wasipatwe na virusi vya
HPV na kupelekea kupatwa na saratani ya mlango wa kizazi ugonjwa ambao ni
hatari na unaua wanawake wengi katika nchi zinazoendelea.
Naye Mratibu wa chanjo wa wilaya Ally Msopa,akitoa mada kwa
washiriki aliwaeleza umuhimu wa chanjo ya HPV kuwa inakinga maambukizi ya
virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi na inatolewa mara
mbili ili kupata kinga kamili,chanjo hii inaweza kupunguza matukio ya saratani
ya mlango wa kizazi kwa kiwango kikubwa.Chanjo hii ni salama,imethibitishwa na
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto na Shirika la afya Duniani.
Aidha Msopa alifafanua baadhi ya dalili za awali za maabukizi ya virusi vya HPV kuwa ni
vivimbe sehemu za uke au uume vijulianavyo kama viotea,dalili za baadaye ni
mabadiliko katika seli za mlango wa kizazi na mabadiliko haya yasipodhibitiwa
mapema hugeuka kuwa saratani ya mlango wa kizazi au viungo vingine.
Kwa upande wake kiongozi wa dini ya kiislamu Sheikh Hamis
Nassor kwa niaba ya viongozi wa dini alisema tumepokea mkakati huu wa serikali
kwa mikono miwili tutahamasisha jamii kwa nguvu zote ili kuwanusuru mabinti
zetu na janga la saratani ya mlango wa kizazi, na kila changamoto
itakayojitokeza tutakabiliana nayo.”Naomba Mungu awajalie viongozi wetu afya
njema umri wenye tija katika kulitumikia taifa”.Sheikh Nassor alisema.
Mkuu wa wilaya katika hotuba yake ya uzinduzi wa kamapeni ya
chanjo ya kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi aliwataka watumishi wa idara ya
afya kuwa na moyo wa uzalendo na wa kujitolea ili zoezi hili liweze kufanikiwa
kwani kuna zahanati ambazo hazina watumishi wa afya na vijiji vingine havina
kabisa zahanati, hivyo alimtaka Mganga wa Halmashauri kuendesha zoezi hili kwa
njia ya huduma ya Vikoba (Out Reach Services)kwa kupanga ratiba za kuwafikia
wananchi katika maeneo yao kwa muda mahsusi ili tuweze kukamilisha zoezi hili
kwa asilimia 100.Baada ya nasaha zake alizindua rasmi kampeni ya chanjo kwa
watoto wa kike wote waliofikia umri wa miaka 14.