Monday, August 14, 2017

Serikali inavyoboresha huduma kwa kutumia mifumo ya Tehama

Na Ofisi ya Habari, Kishapu
Sehemu ya majengo ya hospitali ya wilaya Kishapu

Serikali inatekeleza dhamira yake ya kuhakikisha inawapa wananchi huduma bora kwa wakati na ufanisi ili kuboresha maisha yao kielimu, kiafya na kiuchumi.

Hayo yanafanyika kwa ushurikiano mkubwa na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi ili kufanikisha utoaji huo wa huduma hizo muhimu za kijamii.

Inatoa kipaumbele katika huduma za afya na elimu zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha maisha yao kwani afya na elimu bora kwa wananchi ndiyo raslimali muhimu kwa maendeleo.

Maendeleo ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na elimu na wenye uwezo wa kuzalisha mali. Katika kuhakikisha hilo Serikali imeendelea kushirikiana na  wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.

Hivi karibuni Serikali ilizindua mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma au Public Sector Systems Strengthening (PS3) ukiwa na lengo kusaidia kufanikisha utoaji huduma bora hasa kwa wananchi walioko maeneo ya pembezoni.

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID) inatekeleza mradi huo ikishirikiana na wizara zinazosimamia sekta za afya, elimu na rasilimali fedha.
Utekelezaji wa mfumo huo unaolenga kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na elimu, unatarajiwa kuanza rasmi Julai 2017 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya na elimu ambavyo vipo mikoa 13 inayotekeleza mradi huo.
Katika utoaji huduma hizi mashuleni au vituo vya kutolea huduma za afya vikiwemo hospitali au zahanati suala la matumizi ya rasilimali fedha halikwepeki.

Hii ni kutokana na umuhimu wake kwani ni sehemu ambazo hufanyika manunuzi mbalimbali yakiwemo ya vitendea kazi vya kufundishia, kujifunzia, vya kutolea tiba na dawa.

Hivyo ni muhimu kuwepo na usimamizi wa mzuri ili kuhakikisha fedha hizo zinazotolewa na Serikali kuwahudumia wananchi zinatumika kwa usahihi kwa maana ya ‘value for money’.

Kupitia mfumo huo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa au Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) utasaidia utekelezaji wa utoaji wa rasilimali fedha moja kwa moja vituo vya kutolea huduma.

Hii ni katika kuimarisha uhitaji wa kuwepo kwa usimamizi wa fedha katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma hizo za afya na elimu katika maeneo mbalimbali ya halmashauri.  

Mfumo wa FFARS utaweza kuwapatia watoa huduma mfumo rahisi ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao.  

Hivyo ufuatiliaji matumizi ya fedha hizo utakuwa rahisi katika kufikia malengo ya utoaji huduma na kuhakikisha yanaendana na sheria za ununuzi na utoaji taarifa. 

Taarifa hizi zitasaidia Serikali kuimarisha mfumo wa usimamizi wa fedha za umma na kuongeza uwazi hivyo watoa huduma watawajibika kwa  na wajibu kwa jamii wanayoihudumia.

Mfumo utatumika katika vituo vyote vya kutolea huduma ya afya na shule, na uhuishaji huu wa mfumo utarahisishia na kuongeza ufanisi katika mifumo ya Serikali ya Tanzania na kuboresha usimamizi na matumizi ya rasilimali za umma.

Ili kuhakikisha watoa huduma hizo muhimu, wadau ambao ni watoa huduma za afya na elimu hivi karibuni walipatiwa mafunzo mahsusi ili kuwajengea uwezo katika uhasibu na utoaji taarifa (FFARS).
Kwa kuanzia, Serikali inatarajia kuanza kuutekeleza mfumo mfumo huo mikoa 13 katika halmashauri zake 93 ambapo Shinyanga ni miongoni mwa mikoa hiyo kupitia halmashauri zake zote sita.
Katika makala haya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga iliyonufaika na mradi huo anazungumzia kwa kina kuhusu mfumo wa FFARS.

Anatanabaisha kuwa unasaidia upatikanaji wa taarifa sahihi katika hesabu za mapato na matumizi katika halmashauri zetu tofauti na ilivyokuwa zamani.

Magoiga anasema kuwa kuundwa kwa mfumo huu kutasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku zinasimamiwa vizuri na taarifa za matumizi yake zinatolewa kwa usahihi.

Anaongeza kuwa utaratibu huu mpya utakuwa ni kichocheo cha uwazi na uwajibika wa watendaji wa Serikali ambao ndio watoji wa huduma katika sekta za afya na elimu kwa wananchi.

Hii ni kutokana na kuwa vituo hivyo vya kutolea huduma vinakuwa na mfumo maalumu wa kuandaa taarifa za mapato na matumizi tofauti na ilivyokuwa zamani.

Ni dhahiri kuwa Serikali ina nia ya dhati ya kutoa hudumia bora kwa wananchi wake kwa ufanisi na hilo ndilo lengo lake linalotarajiwa kupitia fedha hizo.

Mkurugenzi mtendaji huyo anasema ni kweli kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali fedha katika vituo vya huduma.

Anasema kuwa kutokana na changamoto hiyo halmashauri hushindwa kutoa taarifa sahihi za matumizi ya ruzuku zinazotolewa katika vituo hivyo na wakati mwingine kusababisha hamashauri husika kupata hati ya mashaka kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Awali hakukuwa na mfumo sahihi wa kusaidia kulizuia hilo lakini kwa mfumo huu mpya sasa utasaidia kuhakikisha kunakuwa na muundo maalumu wa kuhifadhi taarifa za mapato na matumizi.

“Naamini hii itaongeza uwazi na uwajibikaji wa vituo hivi vya kutolea huduma na hivyo kupunguza changamoto mbalimbali ambazo zilikuwepo awali,” anasema. 

Mfumo huo kielektroniki ili kuendana na wakati na mabadiliko ya teknolojia ambapo unafanya kazi sambamba ujazaji vitabu ulioboreshwa.

Hii ni katika kuweza kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo umeme na kutokuwa na upatikanaji wa mtandao kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma katika halmashauri mbalimbali.

Aidha, mara baada ya kujaza katika vitabu, takwimu hizo zitaingizwa katika mfumo kwenye ngazi ya Halmashauri na vituo kupatiwa taarifa ya vituo vyao.

Ni dhahiri kuwa vituo hivyo vitatoa taarifa sahihi ya mapato na matumizi ambazo zitasaidia mwananchi kuhoji pale atakapoona kuwa huduma zinazotarajiwa kupatikana katika vituo hazitolewi kulingana na ruzuku iliyotolewa.

Mradi wa PS3 umefanikishwa na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.