Tuesday, November 7, 2017

DHAMANA NI HAKI YAKO YA KIKATIBA NA KISHERIA

Msomaji wangu kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya watu kupata shida Mara wanapokuwa wametuhumiwa na makosa mbalimbali ya kisheria,hivyo kupata taabu namna ya kupata dhamana hata kukaa rumande pasipo sababu za msingi kana kwamba wamepatikana na hatia.
Dhamana ni kitendo cha mshitakiwa kupewa haki ya kuwa huru wakati polisi inaendelea na uchunguzi wa Kesi yake,wakati Kesi yake inaendelea Mahakamani au wakati akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake. Dhamana ni haki ya kikatiba ya mshitakiwa. Ibara ya 13(6)(b) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inaeleza kuwa " Ni marufuku kwa MTU aliyeshiyakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama MTU mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda kosa hilo". Kumnyima mshitakiwa dhamana,wakati ana haki na anastahili kudhaminiwa kwa mujibu wa sheria,ni sawa na kumtendea kama MTU mwenye kosa hilo,wakati mahakama bado haijathibitisha kuwa ana hatia. Hata hivyo ibara ya 15(1) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,1977 inaeleza wazi kuwa " Kila MTU anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama MTU huru". Kitendo cha kumnyima mshitakiwa dhamana wakati anapaswa kupewa dhamana Ni uvunjifu wa Katiba na kumnyima mshitakiwa haki yake ya kikatiba ya kuwa huru.
MAENEO MATATU YANAYOPELEKEA MTUHUMIWA KUPEWA DHAMANA
1. Wakati upelelezi wa tuhuma dhidi ya mtuhumiwa unaendelea. Hapa Ni wakati mshitakiwa yupo katika Kituo cha polisi,yaani hajafikishwa Mahakamani. Hii Ni kwa mujibu wa kifungu cha 64 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 1985 sura ya 20.
2. Wakati Kesi inaendelea Mahakamani. Hii Ni kwa mujibu wa kifungu cha 148 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 1985.
3. Wakati mshitakiwa aliyetiwa hatiani na mahakama,anapokata rufaa katika mahakama ya juu yake. Katika mazingira hayo mshitakiwa anaweza kupewa dhamana wakati akisubiri maamuzi ya mahakama ambayo amekata rufaa. Hii Ni kwa mujibu wa kifungu cha 368 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 ya mwaka 1985.
MAZINGIRA YANAYOPELEKEA MSHITAKIWA ASIPEWE DHAMANA
Kwa mujibu wa kifungu cha 148(5) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 1985 kinaeleza mazingira hayo kama ifuatavyo:
1. Endapo mshitakiwa ameshshitakiwa kwa kosa la mauaji,uhaini,,wizi wa kutumia silaha na kunajisi.
2. Endapo mshitakiwa ameshitakiwa kwa kosa linalohusiana na madawa ya kulevya.
3. Endapo mshitakiwa aliwahi kufungwa kifungu cha zaidi ya miaka 3.
4. Endapo mshitakiwa aliwahi kupewa dhamana na hakufuata masharti ya dhamana.
5. Mahakama ikiona Ni vyema mshitakiwa aendelee kukaa rumande kwa ajili ya Usalama wake.
Mwisho unapaswa kutambua kuwa dhamana Ni haki yako ya kikatiba na kisheria. Ni jukumu lako kufuata masharti yatakayowekwa na polisi au mahakama ili uweze kupata haki hiyo mpaka mwisho wa Kesi yako.