Tuesday, November 13, 2018

MASWALI NA MAJIBU BUNGENI LEO TAREHE 13/11/2018

Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania


#Akaunti ya pamoja ya fedha kwa ajili ya miamala ya Muungano haijafunguliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika- Dkt. Ashatu Kijaji

#Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha kituo cha Forodha Isongole mpakani mwa Tanzania na Malawi kwa lengo la kutatua changamoto ya mwingiliano wa kibiashara- Dkt. Ashatu Kijaji

#Serikali imewasilisha rasmi maombi ya kufungua Kituo cha Forodha Isongole kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Julai, 2018- Dkt. Ashatu Kijaji

#Sababu zinazoifanya Tanzania isitie au ichelewe kuweka saini na kuridhia Mkataba wa Afrika kuhusu Demokrasia, Chaguzi na Utawala Bora ni kutokana na uwepo wa Ibara ambazo zipo kinyume na Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria zetu- Dkt. Damas Ndumbaro

#Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishiriki kikamilifu katika mchakato wote wa kuandaa wimbo wa Jumuiya ya Afrika Masharimi- Dkt. Damas Ndumbaro.

#Serikali kupitia maonesho mbalimbali ikiwemo maonesho ya Sabasaba na SIDO na kwa kupitia kongano za alizeti imekuwa ikiwakutanisha wakulima wa alizeti, watafiti na wazalishaji wa mafuta wa ndani na nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya soko la alizeti na mafuta kwa ujumla- Mhandisi Stella Manyanya.

# Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Mpango Mkakati wa kuboresha Sekta ya Uvuvi ambao unalenga kuboresha uvuvi nchini ikiwemo kutoa elimu ya uvuvi wa kisasa kwa wavuvi, kuboresha zana za uvuvi na kusambaza teknolojia za uvuvi-Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi.

#Rai yangu kwa wananchi ni kujitahidi kwa nguvu zote kujikinga na maradhi ya magonjwa sugu kwa kula mlo unaofaa, kufanya mazoezi mara kwa mara, kutokutumia tumbaku na kuacha matumizi ya pombe- Mhe. Ummy Mwalimu.

#Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani mwa nchi hususani katika kuimarisha ulinzi na usalama- Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano.

#Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme( TEMESA) katika Mpango wa bajeti ya mwaka wa fefha 2018/2019 imepanga kununua kivuko kwa ajili ya usafiri wa majini katika Bahari ya Hindi kati ya Nyamisati na Kilindoni (Mafia) Mkoani Pwani ili kutoa huduma- Mhe. Elias Kwandikwa

#Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kuwa usimamizi na uendeshaji wa Mitihani inafuata Sheria, Kanuni  na Taratibu zilizopo katika ngazi zote za Elimu-  Mhe. William Ole Nasha

#Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa wanaobainika na kujihusisha na vitendo vya kikatili au unyanyasaji dhidi ya watoto kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi na Sheria za nchi- Mhe. Wiliam Ole Nasha.

*Imeandaliwa na Idara ya habari- MAELEZO*