Monday, February 25, 2019

Chezea Mshahara Usichezee Kazi-Mwanjelwa


“Chezea mshahara usichezee kazi“kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt Mary Mwanjelwa alipokuwa katika kikao alichofanya na watumishi wa Umma katika halmashauri ya Wilaya ya Chalinze,Naibu waziri katika hotuba yake iliyokuwa imesheheni maadili kwa misingi ya kuwafunda watumishi wa kada mbalimbali katika halmashauri hiyo.
   Mwanjelwa katika hotuba yake iliyochukua takribani muda wa dakika 57 aliwataka watumishi wa Umma nchini kuzingatia sheria,taratibu na kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao bila upendeleo wowote,kwa kuwataka wakuu wa idara katika Mamlaka za serikali za mitaa kuwaongoza wasaidizi wao kwa mujibu sheria na kuondokana na utendaji wa mazoea usiokuwa na tija na kuwapa tahadhari endapo watashindwa kuwasimamia waliochini yao watawajibika kwa mujibu wa sheria maana wao ndiyo wamepewa dhamana ya kuongoza.
   Kwa upande wa wasaidizi katika kada mbalimbali,Naibu waziri aliwataka kuheshimu na kutekeleza maelekezo ya viongozi wao pasipo kusukumwa kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma.
    Aidha Mwanjelwa aliwaonya wakuu wa idara kuondokana na kasumba za kujikweza na kujiinua ili kuwakandamiza wasaidizi wao katika kazi kukemea tabia ya "Kujimwambafy" au kujikweza kinyume na sheria za Utumishi wa Umma ili kuwanyanyasa na kuwakandamiza watumishi wa Chini na ikibainika kuna tabia kama hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Kiongozi huyo." Chezea Mshahara usichezee kazi"Mwanjelwa alisisitiza“.
    Kwa upande wa Madiwani kama wasimamizi Wa halmashauri Naibu waziri aliwataka kuzingatia sheria taratibu na kanuni katika maamuzi mbalimbali wanayoyafanya kwa upande wa watumishi na kutenda haki pasipo uonevu,hivyo maamuzi yafanyike kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
     Katika kikao hicho kilichofurika watumishi wa kada mbalimbali Naibu waziri alizungumzia stahiki mbalimbali za watumishi wa Umma na kuwataka waajiri kushughulikia maslahi ya watumishi kwa umakini kwa kuziandaa nyaraka za watumishi kwa usahihi pasipo kukosea kabla ya kuzituma menejimenti ya Utumishi wa Umma."Nyaraka zikiandaliwa kwa usahihi menejimenti ya Utumishi wa Umma haichelewi kutekeleza, hIvyo waajiri andaeni taratibu za watumishi kwa usahihi ili stahiki zao zisipotee“Mwanjelwa alifafanua.
     Mwisho naibu Waziri aliwataka watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuwa wazalendo na waadilifu kwani serikali ya awamu ya tano chini Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ni ya uadilifu na si vinginevyo, chezea mshahara usichezee kazi.