Wednesday, March 28, 2018

Milioni 400 kuondoa kero ya afya Lugoba

Ujenzi wa nyumba ya mganga katika kituo cha afya Lugoba wilayani Chalinze

Ujenzi wa wodi ya mama na mtoto katika kituo cha afya Lugoba

Na John Mlyambate
Kero ya ukosefu wa huduma za afya kubaki historia kwa wananchi wa kata ya Lugoba na maeneo yanayozunguka eneo hilo,kauli hiyo imetolewa na wakazi wa kijiji cha Lugoba hivi karibuni baada ya serikali ya awamu ya tano kutoa fedha shilingi za kitanzania milioni 400 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya huduma za afya kwa maana ya maabara,jengo la upasuaji,jengo la mama na mtoto,jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mganga.
Mwanahabari wa halmashauri alipokuwa akitembelea kituo cha afya Lugoba alikutana na wanachi waliokuwa wakipata huduma ya matibabu kituoni hapo ndipo walipopaza sauti na kusema “Sasa Lugoba kero ya huduma za afya siyo hoja”.Kauli hii ilitolewa na Bi Pili Haji na kushangiliwa na wagonjwa waliokuwa mahali pale kuashiria kero imepata ufumbuzi.
Pili aliendelea kwa kueleza kuwa baada ya kukamilika kwa majengo haya hakutakuwa na sababu ya wananchi kwenda hospitali ya wilaya Bagamoyo au hospitali teule ya  mkoa wa Pwani Tumbi kwani mpaka sasa ikitokea mama mjamzito ameshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida inabidi apelekwe hospitaki ya Tumbi kitu ambacho ni hatari kwa akina mama wajawazito.
Naye Bi Mwajabu Makame mkazi wa kijiji cha Lugoba allishukuru serikali kwa hatua inazoendelea nazo katika kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa afya bora,ili kunusuru maisha ya mama na mtoto katika kata yetu na Chalinze kwa ujumla.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa halmashauri ya Chalinze Dkt.Rahim Hangai akiwa eneo la ujenzi alifafanua kuwa,ujenzi huu wa miradi ya afya unatarajiwa ukamilike mapema na kwa wakati kwani fedha kwa ajili ya mradi huu ipo na inaendelea kutumika na muda si mrefu miundombinu hii itakamilika na kuanza kutumika kama yalivyo malengo ya serikali kuhusu afya.