Sunday, April 29, 2018

Usafi wa kina wafanyika Chalinze


Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya  Chalinze,wafanyakazi na wananchi wa mamlaka ya mji mdogo wa Chalinze wameweza kutekeleza kwa vitendo agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samiah Suluhu Hassan la kufanya usafi wa mazingira kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi,Wananchi hawa wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji ,Bwana Edes Lukoa wamefanya usafi katika kituo cha afya Chalinze,stendi ya mabasi na soko kuu la Chalinze kwa kuzibua mitaro na kuzoa taka kwa kutumia lori la kuzolea taka,zoezi hili limefanyika jana Jumamosi kwa mwitikio wa hali ya juu.
Mkurugenzi wa Hlmashauri ya Chalinze akifanya usafi na wananchi wa Chalinze

Baada ya shughuli ya usafi wananchi wa chalinze na wafanyabiashara wa soko la chalinze linalojulika kwa jina la Soko la kwa Mama Kaguo waliwasilisha maombi yao kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya  Chalinze kutaka wajengewe soko ambalo litakuwa na mgawanyo mzuri kwa wafanyabiashara  kulingana na bidhaa wanazouza katika soko hilo,kupitia kwa Mjumbe wa kamati ya usafi ya soko Bwana Abdulratif Gama alisema”Kwa sasa hakueleweki lipi ni soko kuu na yapi ni masoko madogomadogo kwani hivi sasa tuna masoko matatu,hapa tulipo kwa Mama Kiguo,kuna soko jingine lijulikanalo kama kwa Kassim na soko la Shaabani Nguruka ,hivyo tunaomba tuwe na eneo maalum kwa ajili ya soko”.
Naye Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Lucas Lufunga aliungana na mawazo ya wakazi wa kata yake ya Bwilingu na kuomba halmashauri iweke mikakati ya kujenga soko jipya la wilaya kwani hivi sasa Chalinze ni halmashauri lakini pia ni mamlaka ya mji mdogo ina hitaji kuwekewa mipango mizuri na endelevu kwa maendeleo endelevu kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri Bwana Lukoa aliwataka wafanyabiashara kuwa na utamaduni wa kufanya usafi kila siku na hususan siku hii ya usafi kitaifa ambayo imepangwa na serikali kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe ni siku ya usafi,kila mwananchi katika siku hii atekeleze wajibu wake kuanzia asubuhi saa moja hadi saa nne asubuhi hili ni agizo kila mwananchi anatakiwa kutii.”Nawakumbusha tena kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi wananchi mjitokeze kufanya usafi na hili lizingatiwe bila kupuuzwa”
Hata hivyo Bwana Lukoa alitoa ufafanuzi kuhusu uanzishwaji wa soko la kisasa na kituo cha mabasi kwa hapa Chalinze”Halmashauri inaendelea na mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko na kituo cha mabasi hivyo tuvute subira katika hili na tuzingatie usafi kwa hali tuliyo nayo kwa sasa”.Lukoa alisema.
Usafi katika kituo cha afya cha Chalinze siku ya usafi kitaifa

Wananchi wa Chalinze wakiwa katika barabara kuu iendayo Dar es salaam wakizibua mitaro katika barabara wakiongozwa na Mkurugenzi wa Chalinze Bwana Edes Lukoa