Sunday, April 29, 2018

Kata 12 kukaguliwa utekelezaji wa ilani ya CCM Chalinze


Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani Bagamoyo imekagua jumla ya miradi ya maendeleo 20  katika kata 12 za halmashauri ya wilaya ya Chalinze hivi karibuni, miradi hiyo ni afya 10, elimu 5,viwanda 2,ofisi za watendaji 2 na soko 1,ikiwa ni moja ya kazi ya kamati hiyo kukagua na kuona utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2015-2020 inayotekelezwa kwa sasa nchini kote.
Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo ilikagua na kuona shughuli katika kiwanda cha vigae cha Twyford LTD kilichopo katika kijiji cha Pingi kata ya Pera katika halmashauri ya Chalinze

Kiwanda cha Vigae katika halmashauri ya Chalinze

Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo

Katika ziara hiyo iliyolenga kufuatilia kwa kina utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM wajumbe walijikita zaidi katika kufuatilia ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii kwa maana ya afya, elimu,maji,nyumba za watumishi na kubaini ikama ya watumishi kwa kila kada.Hali kadhalika wajumbe wa kamati hiyo walitaka kufahamu namna ya utoaji huduma kwa wananchi katika maeneo waliyokagua ili kuona yaliyoahidiwa katika ilani kama yanatekelezeka kwa vitendo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Abdul-Rashid Zahor aliwataka wajumbe kukagua kwa kina na kubaini upungufu katika utekelezaji wa Ilani ya chama kwa mujibu wa ibara ya ya 49 hadi ya 58 inayo zungumzia sekta ya huduma za jamii.”Mwaka 2015 tuliahidi kwa wananchi kuboresha huduma za jamii kwa kuwahakikishia uwepo wa huduma bora za afya,elimu na maji,hivyo hatunabudi kuzisimamia halmashauri ili zitekeleze kwa wakati na bila kuchelewa kwani 2019 tutasimama kwa wananchi watatuhoji hivyo hatuko tayari kuhojiwa na kukosa majibu”Zahor alisema.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Kombo Kamote alifafanua kuwa katika ziara hii tulipanga kukagua miradi katika kata zote 15 za halmashauri ya Chalinze lakini hadi sasa tumeweza kuzifikia kata 12 na kutembelea miradi ya afya Lugoba,Msoga,Ubenazomozi,Mdaula,Chalinze,Buyuni,Changalikwa,Rupungwi,Kimange na Miono.Katika ziara hii tumebaini miradi ipo katika hatua mbalimbali ya ujenzi na inaendelea vizuri kwani mingine ni ya kumalizia na mingine bado iko katika hatua za msingi.Kwa upande wa sekta ya elimu tumekagua na kuona miradi katika shule za sekondari Chalinze,Changalikwa,Kimange,Kikaro na shule ya msingi Mbala.Katika elimu tumekagua ujenzi wa maabara,mabweni,nyumba za walimu,madarasa na bwalo,kwa upande wa viwanda tumeweza kukagua na kuona jinsi sekta binafsi zilivyolipokea tamko la serikali kuhusu viwanda kwa kuona uzalishaji katika kiwanda cha vigae kiitwacho “Twyford LTD”kilichopo katika kijiji cha Pingo kata ya Pera,kiwanda hiki kinazalisha vigae bora hapa nchini na kinauza vigae ndani na nje ya nchini kimeweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 900.Vilevile kamati ilitembelea kiwanda cha kuzalisha  vinywaji vinavyotokana na matunda mbalimbali kiitwacho” SAYONA FRUITS”kilichopo katika kijiji cha Msoga kata ya Msoga kiwanda hiki bado kinaendelea kujengwa na muda si mrefu kitaanza kufanya kazi na kitatoa ajira kwa wananchi.
Aidha Kamote alibainisha changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Ilani ikiwa ni pamoja na upungufu wa nyumba za watumishi wa sekta za afya na elimu,upungufu wa watumishi wa sekta hizi kwa upande wa elimu kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati hii imedhihirika baada ya kamati ya siasa kutembelea shule ya sekondari ya Changalikwa ambayo ilibainika kuwa na mwalimu mmoja wa hisabati kwa shule nzima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,Bwana Deogratius Lukomanya alizipokea changamoto zilizobainika katika ziara hiyo ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi zile zilizo ndani ya uwezo wa halmashauri na zile zinazohitaji utekelezaji wa serikali kuu kuzipeleka panapohusika kwa hatua zaidi.
Katika hitimisho wajumbe wa kamati ya siasa waliipongeza halmashauri kwa kutekeleza miradi mingi kwa kutumia mapato ya ndani ni uzalendo wa hali ya juu katika hili na wakaitaka halmashauri kuendelea kufanyakazi kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ambayo ndiyo dira ya maendeleo kwa wanachalinze na watanzania kwa ujumla.