Monday, February 25, 2019

Chezea Mshahara Usichezee Kazi-Mwanjelwa


“Chezea mshahara usichezee kazi“kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt Mary Mwanjelwa alipokuwa katika kikao alichofanya na watumishi wa Umma katika halmashauri ya Wilaya ya Chalinze,Naibu waziri katika hotuba yake iliyokuwa imesheheni maadili kwa misingi ya kuwafunda watumishi wa kada mbalimbali katika halmashauri hiyo.
   Mwanjelwa katika hotuba yake iliyochukua takribani muda wa dakika 57 aliwataka watumishi wa Umma nchini kuzingatia sheria,taratibu na kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao bila upendeleo wowote,kwa kuwataka wakuu wa idara katika Mamlaka za serikali za mitaa kuwaongoza wasaidizi wao kwa mujibu sheria na kuondokana na utendaji wa mazoea usiokuwa na tija na kuwapa tahadhari endapo watashindwa kuwasimamia waliochini yao watawajibika kwa mujibu wa sheria maana wao ndiyo wamepewa dhamana ya kuongoza.
   Kwa upande wa wasaidizi katika kada mbalimbali,Naibu waziri aliwataka kuheshimu na kutekeleza maelekezo ya viongozi wao pasipo kusukumwa kwa mujibu wa sheria za Utumishi wa Umma.
    Aidha Mwanjelwa aliwaonya wakuu wa idara kuondokana na kasumba za kujikweza na kujiinua ili kuwakandamiza wasaidizi wao katika kazi kukemea tabia ya "Kujimwambafy" au kujikweza kinyume na sheria za Utumishi wa Umma ili kuwanyanyasa na kuwakandamiza watumishi wa Chini na ikibainika kuna tabia kama hiyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya Kiongozi huyo." Chezea Mshahara usichezee kazi"Mwanjelwa alisisitiza“.
    Kwa upande wa Madiwani kama wasimamizi Wa halmashauri Naibu waziri aliwataka kuzingatia sheria taratibu na kanuni katika maamuzi mbalimbali wanayoyafanya kwa upande wa watumishi na kutenda haki pasipo uonevu,hivyo maamuzi yafanyike kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.
     Katika kikao hicho kilichofurika watumishi wa kada mbalimbali Naibu waziri alizungumzia stahiki mbalimbali za watumishi wa Umma na kuwataka waajiri kushughulikia maslahi ya watumishi kwa umakini kwa kuziandaa nyaraka za watumishi kwa usahihi pasipo kukosea kabla ya kuzituma menejimenti ya Utumishi wa Umma."Nyaraka zikiandaliwa kwa usahihi menejimenti ya Utumishi wa Umma haichelewi kutekeleza, hIvyo waajiri andaeni taratibu za watumishi kwa usahihi ili stahiki zao zisipotee“Mwanjelwa alifafanua.
     Mwisho naibu Waziri aliwataka watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kuwa wazalendo na waadilifu kwani serikali ya awamu ya tano chini Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ni ya uadilifu na si vinginevyo, chezea mshahara usichezee kazi.






Tuesday, November 13, 2018

MASWALI NA MAJIBU BUNGENI LEO TAREHE 13/11/2018

Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania


#Akaunti ya pamoja ya fedha kwa ajili ya miamala ya Muungano haijafunguliwa na kuanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika- Dkt. Ashatu Kijaji

#Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha kituo cha Forodha Isongole mpakani mwa Tanzania na Malawi kwa lengo la kutatua changamoto ya mwingiliano wa kibiashara- Dkt. Ashatu Kijaji

#Serikali imewasilisha rasmi maombi ya kufungua Kituo cha Forodha Isongole kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Julai, 2018- Dkt. Ashatu Kijaji

#Sababu zinazoifanya Tanzania isitie au ichelewe kuweka saini na kuridhia Mkataba wa Afrika kuhusu Demokrasia, Chaguzi na Utawala Bora ni kutokana na uwepo wa Ibara ambazo zipo kinyume na Katiba ya Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria zetu- Dkt. Damas Ndumbaro

#Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishiriki kikamilifu katika mchakato wote wa kuandaa wimbo wa Jumuiya ya Afrika Masharimi- Dkt. Damas Ndumbaro.

#Serikali kupitia maonesho mbalimbali ikiwemo maonesho ya Sabasaba na SIDO na kwa kupitia kongano za alizeti imekuwa ikiwakutanisha wakulima wa alizeti, watafiti na wazalishaji wa mafuta wa ndani na nje ya nchi ili kukidhi mahitaji ya soko la alizeti na mafuta kwa ujumla- Mhandisi Stella Manyanya.

# Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa Mpango Mkakati wa kuboresha Sekta ya Uvuvi ambao unalenga kuboresha uvuvi nchini ikiwemo kutoa elimu ya uvuvi wa kisasa kwa wavuvi, kuboresha zana za uvuvi na kusambaza teknolojia za uvuvi-Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi.

#Rai yangu kwa wananchi ni kujitahidi kwa nguvu zote kujikinga na maradhi ya magonjwa sugu kwa kula mlo unaofaa, kufanya mazoezi mara kwa mara, kutokutumia tumbaku na kuacha matumizi ya pombe- Mhe. Ummy Mwalimu.

#Serikali inatambua umuhimu wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani mwa nchi hususani katika kuimarisha ulinzi na usalama- Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano.

#Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme( TEMESA) katika Mpango wa bajeti ya mwaka wa fefha 2018/2019 imepanga kununua kivuko kwa ajili ya usafiri wa majini katika Bahari ya Hindi kati ya Nyamisati na Kilindoni (Mafia) Mkoani Pwani ili kutoa huduma- Mhe. Elias Kwandikwa

#Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha kuwa usimamizi na uendeshaji wa Mitihani inafuata Sheria, Kanuni  na Taratibu zilizopo katika ngazi zote za Elimu-  Mhe. William Ole Nasha

#Serikali imeendelea kuchukua hatua kwa wanaobainika na kujihusisha na vitendo vya kikatili au unyanyasaji dhidi ya watoto kwa mujibu wa taratibu za kiutumishi na Sheria za nchi- Mhe. Wiliam Ole Nasha.

*Imeandaliwa na Idara ya habari- MAELEZO*

Monday, November 5, 2018

YALIYOJIRI WAKATI MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DKT. HASSAN ABBASI AKITOA TAARIFA YA MAMBO MUHIMU YALIYOTEKELEZWA NA SERIKALI YA AWAMU TANO NDANI YA MIAKA MITATU*

*

#Leo Novemba 5, 2018 ni miaka mitatu ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano; ni zaidi kidogo ya nusu ya muhula wa miaka mitano ya awali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa madarakani.

#Rais Dkt.John Magufuli anawashukuru Watanzania wote ambao wameendelea kuiunga mkono Serikali yake kwa namna mbalimbali ikiwemo kutimiza wajibu wao kama vile kulipa kodi, kuchapakazi kwa bidii na kuishi kwa maadili.

#Ahadi kuu ya Rais Magufuli  katika miaka ijayo kwa watanzania wote ni kuwa yeye binafsi na Serikali yake nzima wataendeleza mageuzi ya kweli ambayo leo hapa tutaangalia baadhi ya mafanikio yake.

#Rais Magufuli Anawaomba muendelee kumuombea yeye binafsi na Serikali yake, kudumisha, amani na kila mtu awe na upendo na uzalendo kwa Taifa lake.

#Miaka mitatu leo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi wa dunia na hata ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania chini ya Rais Magufuli imeendelea kuwa na uchumi unaoendelea kukua kwa kasi nzuri.

#Katika mwaka 2017/18 uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 7.1 na kuongoza katika nchi zote za Afrika Mashariki lakini ukiingia katika rekodi ya kuwa miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi zaidi duniani kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kimataifa.

#Katika miaka hii mitatu Rais Magufuli amethubutu kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza kasi ya kukusanya kodi na hivyo kuongeza mapato ya kodi ya Serikali kutoka wastani wa TZS Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia wastani wa TZS Trilioni 1.3 kwa mwezi.

#Kutokana na ufuatiliaji, ubunifu, uwekezaji wa Serikali ya Rais Magufuli mashirika mengi ya aina hiyo sasa yameanza kuamka kuwa na ufanisi, kuongeza mapato na mengine kutengeneza faida. Kwa minajali ya muda nitatoa mifano michache kwa Mashirika kama TTCL, TRC, DAWASA na Bandari.

#Rais Magufuli alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita aliahidi kurejesha azma ya tangu wakati wa Baba wa Taifa ya kujenga Nchi ya Viwanda. Katika kipindi hiki viwanda 3,306 viliandikishwa, vinaendelea kujengwa na baadhi vimekamilika na vinatoa bidhaa mbalimbali. Kati ya hivyo 251 ni vikubwa na vya kati ni 173.

#Licha ya mchango kwa Pato la Taifa, masoko na jamii kupata malighafi, ujenzi na kuanza kazi kwa baadhi ya viwanda vipya, tayari kumeanza kusaidia kuwapatia ajira Watanzania. Takwimu za mpaka Juni 30, 2018 zinaonesha kuwa sekta ya uzalishaji viwandani imefikisha ajira 280,899 kutoka ajira 254,785 mwaka 2015.

#Tayari mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 5.2 mwaka 2015 hadi 5.5 mwaka 2017. Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Viwanda ilikua kutoka asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi asilimia 7.1 mwaka 2017/18.

#Viwanda katika miaka hii mitatu vimeongeza ajira kwa zaidi ya Watanzania 26,000 huku ajira nyingine zaidi ya 100,000 zikitarajiwa kuongezeka kupitia uwekezaji wa miradi mbalimbali ipatayo 905 iliyosajiliwa kupitia TIC mingi ikiwa viwanda, majengo, kilimo.

# Rais Magufuli amepambana na rushwa na ufisadi kwa, pamoja na mambo mengine, kutimiza Ahadi yake ya kuunda Mahakama ya Mafisadi.

#Mahakama ya Mafisadi (Makosa ya Uhujumu Uchumi) ilianza kazi rasmi Julai, 2017. Mpaka sasa kesi mpya 41 zilifunguliwakuna na maombi ya dhamana 346 yamewasilishwa katika Mahakama hii kati ya 2007 na 2018.

#Kwa upande wa PCCB nayo imeendelea kwa kasi kuzuia na kupambana na rushwa ambapo kesi mpya 495 zilifunguliwa kati ya mwaka 2016 na 2017 ambapo asilimia 60.14%  walifungwa.

#Takukuru imeokoa TZS Bilioni 70.34 zilizokuwa zilipwe kifisadi na imezuia Bilioni 42.16 na Euro 4.3m mpaka kesi ziishe.

#Baada ya mafanikio ya Serikali kuleta ndege nne mpya zinazoendelea kuleta mageuzi katika usafiri wa anga nchini, abiria wanaotumia ndege za ATCL wameongezeka kutoka takribani abiria 4,000 kwa mwezi hadi abiria 30,000 kwa mwezi.

#Tunaleta AIR BUS  mbili zenye uwezo wa watu 132+ zinawasili nchini Disemba, 2018 na BOEING DREAMLINER ya 2: Hii inakuja nchini Oktoba mwaka 2019.

#Katika kipindi hiki, Serikali imeanza au inajiandaa kutekeleza miradi mikubwa na ya kihistoria kwa maendeleo ya Taifa ikiwemo utandikaji wa reli ya kisas( Standard Guage).

#Serikali imetekeleza miradi muhimu kwa maisha ya watu katika masuala ya Afya, Elimu na Nishati.

#Serikali imeokoa mabilioni ya fedha za wananchi kwa kuwekeza katika uzalishaji wa umeme wa gesi badala ya kutegemea mitamgo ya mafuta. Miradi ya Kinyerezi I-Extension (megawati 185) na Kinyerezi II (megawati 240+) inaelekea kukamilika. Tayari Kinyerezi II peke yake imeshaingiza megawati zaidi ya 200 kwenye gridi ya Taifa.

#Serikali imeongeza bajeti ya fedha za ndani ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoka Shilingi bilioni 290.2 mwaka 2014/15 hadi Shilingi bilioni 375.38 mwaka 2018/19 na na kazi ya Awamu ya Tatu ya Usambazaji Umeme Vijijini imeanza na inaendelea.

#Serikali imewekeza katika sekta ya afya ikiwemo kujenga Vituo vya Afya vya Kata 210 na kukarabati vingine vingi kufikisha idadi ya vituo vinavyotoa huduma hadi mwaka huu kuwa 7,746 kutoka vituo 7,014 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 10.4. Vituo hivi pia vina wodi za kina mama na vifaa vya kisasa. Aidha, ajira zaidi ya 6,000 za kada ya afya zimetolewa.

#Katika miaka mitatu Zahanati zimeongezeka kutoka 6,143 mwaka 2015 hadi 6,646 mwaka huu (Ongezeko la zahanati 503) ambapo baadhi zilijengwa na zingine kukarabatiwa sawa na ongezeko la asilimia 8.1.

#Kazi kubwa imefanyika kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa ikiwemo kununua CT-Scan, MRI, Digital scanners na kuimarisha tiba za kibingwa kama moyo, kupandikiza ini na oparesheni za mifupa, mgongo na masikio (Cochler inplant).  Vifaa hivi vimepunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje kutoka wastani wa 553 mwaka 2015/16 hadi 103 mwaka wa fedha uliopita.

#Kutokana na kuimarika tiba hizi za kibingwa tumeshapokea wagonjwa kutoka nchi za: Komoro, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, DRC, Zambia na wataalam wa nje zinaleta wagonjwa wao kutibiwa Tanzania).

#Serikali imeendeleza jitihada za kuongeza huduma ya maji kwa lengo la kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini. Miradi mikubwa na midogo inaendelea kote nchini.

#Miradi 1,571 yenye jumla vituo vya maji 126,610 imekamilika na baadhi inakamilika, na itakapokamilika yote iliyobaki itafikisha uwezo wa kuhudumia jumla ya watu milioni 31.65 sawa na asilimia 81 ya wakazi waishio vijijini.

#Katika Elimu ya juu Serikali ya Awamu ya Tano imemaliza  migomo isiyo ya lazima kwani si tu Bajeti Elimu ya Juu imepanda hadi TZS Bilioni 427.5 mwaka huu kutoka Bilioni 348 mwaka 2015, fedha hizo sasa zinatoka mapema (Mfano: Bilioni 137 zilishatolewa tangu Septemba mwaka huu kusubiri wanafunzi wapya kupewa fedha za siku 60 za kwanza).

#Katika jitihada za Serikali kuvutia wanafunzi wengi zaidi kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati, si kuimarisha masomo ya sanaa pekee, Serikali inatekeleza mkakati wa kukamilisha maabara 3 za Sayansi katika kila shule.  Kwa sasa shule za Serikali zenye maabara ni 2,141 kati ya 3,614.

#Ukuta wa Mererani umewezesha Serikali kupata mapato kutoka Milioni 71 hadi kufika Bilioni 1.2 .

#Katika miaka hii mitatu licha ya matukio ya hapa na pale, bado Tanzania, imesimama kama moja ya visiwa vya amani duniani na Tanzania.

#Rais Magufuli amesimamia misingi ya Taifa ambapo Watanzania leo tuko huru kuamua mambo yetu kama Taifa, safari ya kujitegemea imeanza na hata Mataifa makubwa na madogo yanafahamu kuna mtu huyu anaitwa JOHN POMBE MAGUFULI na ana azma gani kwa Taifa lake. Miradi aliyoianzisha kwa fedha za ndani ni utekelezaji wa azma hiyo.

#Kama nchi tunapaswa kuendelea kupambana na wanamaslahi mbalimbali ambao hawafurahishwi na mageuzi haya, lazima tuungane kuwapinga na kuendelea kuwapa moyo viongozi wetu.

#Mataifa yaliyofanikiwa yamepita katika vipindi vya mageuzi. Nasi tunapaswa kupitia mkondo huo huo. Mataifa kama China, Malaysia, Indonesia n.k tulikuwa nao karibu sawa leo wako mbali hivyo Tanzania itajengwa na watu wenye kuchapakazi, kujituma, kulipa kodi na kuwa watiifu.

*Imetayarishwa na Idara ya habari- MAELEZO*

Chalinze Eneo Ghafi Tanzania


Halmashauri ya Chalinze kwa Mkoa wa Pwani ni halmashauri ghafi kwa maana kwamba ni kiini cha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini inayotekelezwa kwa kasi.ninaposema ni halmashauri ghafi au eneo ghafi ni eneo lenye madini mbalimbali ya ujenzi kama mchanga,mawe,kokoto na mawe mbalimbali yanayotumika kutengeneza vigae katika viwanda vyetu hapa nchini.
Kwa upande wa kokoto inayopatikana Chalinze ni kokoto bora katika Afrika Mashariki inayotumika katika ujenzi wa reli ya kisasa yaani “Standard Gauge Railway”kokoto hii ni kokoto inayokubalika kimataifa ni kokoto ambayo inatumika katika ujenzi wa reli hii ambayo ni mradi wa kitaifa ambao kimsingi serikali ya awamu ya tano inautekeleza kwa kasi ya hali ya juu,hivyo utekelezaji wa mradi huu hatuwezi kusema tunatekeleza pasipo kuitaja Chalinze.
Aidha tuna mradi mwingine ambao umekwisha kamilika katika jiji la Dar es salaam,mradi wa daraja la juu yaani “Flyover”mradi huu umejengwa kwa kutumia kokoto inayotoka Chalinze kuanzia mwanzo wa ujenzi hadi mwisho,kwa hiyo bado wanachalinze na Pwani kwa ujumla tutaendelea kujivunia Chalinze kama eneo ghafi lenye fursa za kutosha katika kukuza uchumi wa Tanzania kupitia matumizi sahihi ya mali ghafi inayopatikana Chalinze.



 

 

 

 

Kokoto ya Chalinze ni kokoto bora inayotumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya serikali na ya ile sekta binafsi kwa maana ya ujenzi wa nyumba binafsi,majengo ya umma,barabara na madaraja mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini.
Serikali iko katika maandalizi ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji katika bonde la mto Rufiji,mradi ambao utaondoa kero ya upungufu wa umeme nchini.Katika ujenzi wa mradi huu kokoto itakayotumika ni kokoto kutoka Chalinze,kiasi kikubwa cha kokoto kitatumika katika utekelezaji wa mradi huu.
Hivyo dhana ya Chalinze kuwa Eneo Ghafi la utekelezaji wa ujenzi wa miradi mbalimbali ya kitaifa itaendelea kuishi siku zote na tutaendelea kusema” Chalinze Eneo Ghafi,Chalinze kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Ujenzi kitaifa”

Wednesday, May 2, 2018

Chajo ya kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi yazinduliwa rasmi Chalinze


Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Alhaj Majid Mwanga amezindua rasmi kampeni ya chanjo ya kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi kwa watoto wa kike waliofikia umri wa miaka 14,uzinduzi huo umefanyika jana katika kijiji cha Kikaro kata ya Miono katika halmashauri ya wilaya ya Chalinze.Kampeni hizi ni mkakati wa serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ambao umekuwa tishio kwa afya za wanawake hapa nchini na ulimwenguni kote kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga akizindua zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi

Shehe Hamis Nasoro akichangia jambo katika uzinduzi wa

Wanafunzi wa shule ya sekondari Kikaro

Shehe akihamasisha zoezi la chanjo



Kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo kulitolewa mafunzo kwa wadau na wahamasishaji wa masuala ya afya ya msingi katika jamii kwa maana ya wahudumu wa afya,maafisa watendaji wa vijiji na kata,maafisa tarafa,maafisa maendeleo ya jamii,viongozi mbalimbali wa dini na walimu wa shule za msingi na sekondari ili wapate ufahamu kuhusu saratani ya mlango wa uzazi,dalili za maabukizi ya virusi vya “Human Pappiloma Virus”(HPV),dalili za saratani ya mlango wa kizazi,chanjo ya kukinga Saratani ya mlango wa kizazi,namna inavyotolewa chanjo na maudhi madogo madogo yanayoweza kutokea baada ya chanjo kwa watoto.
Katika mafunzo hayo Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya Dkt.Rahim Hangai aliwataka washiriki kuwa mabalozi katika kufanikisha zoezi hili muhimu la kitaifa ili kuwanusuru watoto wa kike wasipatwe na virusi vya HPV na kupelekea kupatwa na saratani ya mlango wa kizazi ugonjwa ambao ni hatari na unaua wanawake wengi katika nchi zinazoendelea.
Naye Mratibu wa chanjo wa wilaya Ally Msopa,akitoa mada kwa washiriki aliwaeleza umuhimu wa chanjo ya HPV kuwa inakinga maambukizi ya virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi na inatolewa mara mbili ili kupata kinga kamili,chanjo hii inaweza kupunguza matukio ya saratani ya mlango wa kizazi kwa kiwango kikubwa.Chanjo hii ni salama,imethibitishwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto na Shirika la afya Duniani.
Aidha Msopa alifafanua baadhi ya dalili za awali  za maabukizi ya virusi vya HPV kuwa ni vivimbe sehemu za uke au uume vijulianavyo kama viotea,dalili za baadaye ni mabadiliko katika seli za mlango wa kizazi na mabadiliko haya yasipodhibitiwa mapema hugeuka kuwa saratani ya mlango wa kizazi au viungo vingine.
Kwa upande wake kiongozi wa dini ya kiislamu Sheikh Hamis Nassor kwa niaba ya viongozi wa dini alisema tumepokea mkakati huu wa serikali kwa mikono miwili tutahamasisha jamii kwa nguvu zote ili kuwanusuru mabinti zetu na janga la saratani ya mlango wa kizazi, na kila changamoto itakayojitokeza tutakabiliana nayo.”Naomba Mungu awajalie viongozi wetu afya njema umri wenye tija katika kulitumikia taifa”.Sheikh Nassor alisema.
Mkuu wa wilaya katika hotuba yake ya uzinduzi wa kamapeni ya chanjo ya kuzuia Saratani ya Mlango wa Kizazi aliwataka watumishi wa idara ya afya kuwa na moyo wa uzalendo na wa kujitolea ili zoezi hili liweze kufanikiwa kwani kuna zahanati ambazo hazina watumishi wa afya na vijiji vingine havina kabisa zahanati, hivyo alimtaka Mganga wa Halmashauri kuendesha zoezi hili kwa njia ya huduma ya Vikoba (Out Reach Services)kwa kupanga ratiba za kuwafikia wananchi katika maeneo yao kwa muda mahsusi ili tuweze kukamilisha zoezi hili kwa asilimia 100.Baada ya nasaha zake alizindua rasmi kampeni ya chanjo kwa watoto wa kike wote waliofikia umri wa miaka 14.

Zingatieni Sheria na maadili ya kazi-RC Pwani


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo awataka waajiri na wafanyakazi kuheshimu sheria za utumishi wa umma kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi,ameyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani yaliyoadhimishwa kimkoa katika halmashauri ya Mji wa Kibaha Jana katika viwanja vya shirika la elimu Kibaha na kukemea tabia za baadhi ya waajiri wasiotaka kufuata sheria za utumishi kwa kunyanyasa wafanyakazi hatakuwa tayari kufanya kazi na watu wa aina hiyo katika mkoa wa Pwani.


Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo(katikati) akiimba wimbo wa wafanyakazi

Wafanyakazi bora wa halmashauri ya wilaya ya Chalinze katika maandamano

Wafanyakazi hodari kutoka halmashauri ya Chalinze wakiwa na furaha kwa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani

Wafanyakazi bora wakiongozwa na afisa utumishi wa Chalinze Ruth Timba

Wafanyakazi hodari wakiwa katika viwanja vya shirika la elimu kibaha

Chalinze Hoyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee

Hoyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee

Hoyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee

Meza kuu wakati wa Mei Mosi 2018

Viongozi mbalimbali katika maadhimisho ya mei mosi 2018

VIongozi mbaimbali

Wafanyakazi hodari baada ya kutunukiwa zawadi zao

Solidarity forever

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chalinze,Bwana Edes Lukoa Akijitambulisha katika kusanyiko la mei mosi

Wafanyakazi hodari wakipeana hongera

Mkuu wa Mkoa wa Pwani akitoa hotuba yake katika siku ya Mei Mosi

Wafanyakazi wa Chalinze ktika picha ya pamoja na Mkurugenzi wao

Picha ya Pamoja baada ya maadhimisho

Akisoma Risala ya shirikisho la wafanyakazi(TUCTA )Mkoani Pwani Bwana Ramadhani Kinyagoli aliishukuru serikali kwa jitihada zake katika shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa maslahi ya watanzania wakiwemo na wafanyakazi,hata hivyo hakusita kuwasilisha madai na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wa mkoa wa Pwani ikiwa ni pamoja na wafanyakazi kutopandishwa vyeo kwa wakati,kodi kubwa ya mshahara,wastaafu kutolipwa mafao yao kwa wakati,waajiri kutoheshimu sheria za utumishi kwa kutowatendea haki watumishi kwa kuwapa maslahi yao kwa mujibu wa sheria,sekta binafsi kuwazuia watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi na baadhi ya halmashauri kutoitisha vikao vya mabaraza ya wafanyakazi.
Kinyangoli aliendelea kufafanua kero zinazowasibu wafanyakazi katika mkoa wa Pwani kwa kutoa shutuma kwa baadhi ya waajiri kutotimiza ahadi zao kwa wafanyakazi hodari wa mwaka jana kwa kutowapa zawadi zao hadi sasa na kuomba Uongozi wa mkoa ulifanyie kazi kwa waajiri hao kwani ahadi zisizotekelezeka kwa wakati huvunja moyo wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na serikali.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo,katika hotuba yake baada ya risala ya wafanyakazi wa mkoa wa Pwani aliwapongeza wafanyakazi hodari kwa mwaka 2018 kwa utendaji mzuri hata wakaweza kuteuliwa kuwa watumishi hodari kutoka katika taasisi zao.Aliendelea kulipongeza shirikisho la wafanyakazi mkoa wa Pwani kwa risala nzuri iliyosheheni mambo mazuri na yenye tija kwa mstakabari wa utumishi nchini na kusema hakika risala hii imejaa “Nondo za kutosha”Ndikilo alisema.
Mheshimiwa Ndikilo katika hotuba yake aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazo wakabili wafanyakazi ambazo ziko ndani ya uwezo wake na kwa zile zilizo nje ya uwezo wake aliahidi kuziwasilisha kunakohusika kwa hatua zaidi. Aliwataka watumishi wa serikali na sekta binafsi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni katika utumishi sanjari na maadili ya kazi kwa mujibu wa taaluma walizonazo.Aliwataka wafanyakazi kujiepusha na matendo ya utovu wa nidhamu katika kazi.”Lazima tuwe na nidhamu ya kazi uvivu kazini ni sumu katika ajira”Ndikilo alisema.
Aidha Ndikilo alisikitishwa na kitendo cha waajiri wanaotoa ahadi hewa kwa watumishi hodari na kutowatunuku zawadi zao kwa wakati hili halikubaliki hata kidogo na kutoa onyo kwa waajiri wanaobagua wananchi katika ajira hususan watu wenye ulemavu na wanawake na alisisitiza sitakuwa tayari kufanya kazi na wawekezaji wa aina hii kwani wanafanya vitu vilivyo kinyume na katiba na sheria za nchi pia.
Mwisho Mkuu wa mkoa aliwataka waajiri kuacha tabia ya kuzuia watumishi kuhama kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine ni haki ya mtumishi hivyo kukubali au kukataa uhamisho ni jukumu la wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa si suala la mwajiri.”Kama mwajiri toa maoni yako katika barua ya mtumishi na siyo kumzuia au kukataa kumpitishia barua yake ni kosa mruhusu na TAMISEMI wataamua”.Ndikilo alisema.

Sunday, April 29, 2018

Kata 12 kukaguliwa utekelezaji wa ilani ya CCM Chalinze


Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani Bagamoyo imekagua jumla ya miradi ya maendeleo 20  katika kata 12 za halmashauri ya wilaya ya Chalinze hivi karibuni, miradi hiyo ni afya 10, elimu 5,viwanda 2,ofisi za watendaji 2 na soko 1,ikiwa ni moja ya kazi ya kamati hiyo kukagua na kuona utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2015-2020 inayotekelezwa kwa sasa nchini kote.
Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo ilikagua na kuona shughuli katika kiwanda cha vigae cha Twyford LTD kilichopo katika kijiji cha Pingi kata ya Pera katika halmashauri ya Chalinze

Kiwanda cha Vigae katika halmashauri ya Chalinze

Wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Bagamoyo

Katika ziara hiyo iliyolenga kufuatilia kwa kina utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM wajumbe walijikita zaidi katika kufuatilia ujenzi wa miundombinu ya huduma za jamii kwa maana ya afya, elimu,maji,nyumba za watumishi na kubaini ikama ya watumishi kwa kila kada.Hali kadhalika wajumbe wa kamati hiyo walitaka kufahamu namna ya utoaji huduma kwa wananchi katika maeneo waliyokagua ili kuona yaliyoahidiwa katika ilani kama yanatekelezeka kwa vitendo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Abdul-Rashid Zahor aliwataka wajumbe kukagua kwa kina na kubaini upungufu katika utekelezaji wa Ilani ya chama kwa mujibu wa ibara ya ya 49 hadi ya 58 inayo zungumzia sekta ya huduma za jamii.”Mwaka 2015 tuliahidi kwa wananchi kuboresha huduma za jamii kwa kuwahakikishia uwepo wa huduma bora za afya,elimu na maji,hivyo hatunabudi kuzisimamia halmashauri ili zitekeleze kwa wakati na bila kuchelewa kwani 2019 tutasimama kwa wananchi watatuhoji hivyo hatuko tayari kuhojiwa na kukosa majibu”Zahor alisema.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Bagamoyo Bwana Kombo Kamote alifafanua kuwa katika ziara hii tulipanga kukagua miradi katika kata zote 15 za halmashauri ya Chalinze lakini hadi sasa tumeweza kuzifikia kata 12 na kutembelea miradi ya afya Lugoba,Msoga,Ubenazomozi,Mdaula,Chalinze,Buyuni,Changalikwa,Rupungwi,Kimange na Miono.Katika ziara hii tumebaini miradi ipo katika hatua mbalimbali ya ujenzi na inaendelea vizuri kwani mingine ni ya kumalizia na mingine bado iko katika hatua za msingi.Kwa upande wa sekta ya elimu tumekagua na kuona miradi katika shule za sekondari Chalinze,Changalikwa,Kimange,Kikaro na shule ya msingi Mbala.Katika elimu tumekagua ujenzi wa maabara,mabweni,nyumba za walimu,madarasa na bwalo,kwa upande wa viwanda tumeweza kukagua na kuona jinsi sekta binafsi zilivyolipokea tamko la serikali kuhusu viwanda kwa kuona uzalishaji katika kiwanda cha vigae kiitwacho “Twyford LTD”kilichopo katika kijiji cha Pingo kata ya Pera,kiwanda hiki kinazalisha vigae bora hapa nchini na kinauza vigae ndani na nje ya nchini kimeweza kutoa ajira kwa watanzania zaidi ya 900.Vilevile kamati ilitembelea kiwanda cha kuzalisha  vinywaji vinavyotokana na matunda mbalimbali kiitwacho” SAYONA FRUITS”kilichopo katika kijiji cha Msoga kata ya Msoga kiwanda hiki bado kinaendelea kujengwa na muda si mrefu kitaanza kufanya kazi na kitatoa ajira kwa wananchi.
Aidha Kamote alibainisha changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Ilani ikiwa ni pamoja na upungufu wa nyumba za watumishi wa sekta za afya na elimu,upungufu wa watumishi wa sekta hizi kwa upande wa elimu kuna upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati hii imedhihirika baada ya kamati ya siasa kutembelea shule ya sekondari ya Changalikwa ambayo ilibainika kuwa na mwalimu mmoja wa hisabati kwa shule nzima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,Bwana Deogratius Lukomanya alizipokea changamoto zilizobainika katika ziara hiyo ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi zile zilizo ndani ya uwezo wa halmashauri na zile zinazohitaji utekelezaji wa serikali kuu kuzipeleka panapohusika kwa hatua zaidi.
Katika hitimisho wajumbe wa kamati ya siasa waliipongeza halmashauri kwa kutekeleza miradi mingi kwa kutumia mapato ya ndani ni uzalendo wa hali ya juu katika hili na wakaitaka halmashauri kuendelea kufanyakazi kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ambayo ndiyo dira ya maendeleo kwa wanachalinze na watanzania kwa ujumla.